Uchaguzi wa mji wa Istanbul Magazetini
24 Juni 2019
Tunaanzia Uturuki ambako matokeo ya uchaguzi uliorudiwa wa baraza la mji wa Istanbul yamethibitisha ushindi wa upande wa upinzani. Hakuna gazeti la Ujerumani ambalo halikuchambua matokeo hayo. "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Matokeo ya uchaguzi sio tu ni ushindi kwa Imamoglu, bali pia ni onyo kwa kiongozi wa nchi hiyo: Erdogan hawezi tena kujinata hawezi kushindwa. Alianza kujipatia umashuhuri mwaka 1994 alipokuwa meya wa Istanbul. Miaka 25 baadae, matokeo hayo ya uchaguzi yanaweza kuashiria mwanzo wa kuporomoka kwake kisiasa. Lakini zaidi kuliko yote, matokeo ya uchaguzi wa jiji la Istanbul ni ushindi kwa mfumo wa demokrasia nchini Uturuki."
Gazeti la Badische Zeitung linajiuliza rais Erdogan na chama chake cha AKP watasema nini tena baada ya matokeo hayo kutangazwa? Gazeti linaendelea kuandika:"Eti watashuku kwa mara nyengine tena? Au Erdogan atatekeleza vitisho alivyotoa vya kumfikisha mahakamani mshindi na kumuapisha badala yake mtu anaemtaka! Uamuzi kama huo sio tu utazusha hasira miongoni mwa wananchi bali pia utaitumbukiza Uturuki katika zahma ya machafuko yasiyokuwa na mfano. Uchaguzi umeshapita, Erdogan anabidi akubali anaweza pia kushindwa."
Vitisho vya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia
Mjadala umepamba moto kufuatia kisa cha kuuliwa meya wa mji wa Kassel katika jimbo la Hesse Wolter Lübcke na mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Chanzo cha mauwaji ni msimamo wake kuelekea wahamiaji. Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu Horst Seehofer anataka wanyimwe haki msingi wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Gazeti la "Badische Meueste Nachrichten" linaandika: "Hiyo sio njia ya maana anayoichonga waziri. Na pengine inaweza kuwa ya hatari. Kwasababu taifa linalofuata sheria limejengeka kwa msingi wa kudhamini haki msingi kwa kila raia, mwanamke kwa mwanamme, kila mgeni, kila mwenye kuomba kinga ya ukimbizi, kila mhalifu na kila mnazi mambo leo. Hilo linaumiza baadhi ya wakati, lakini ni la lazima na hivyo ndivyo taifa linalofuata sheria linavyofanyakazi."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse
Mhariri: Sekione Kitojo