1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Israel: Netanyahu vs Gantz duru ya 3

2 Machi 2020

Waisrael wanapiga kura katika uchaguzi usio wa kawaida na wa tatu nchini humo kuandaliwa katika kipindi cha mwaka mmoja utakaoamua kama Waziri Mkuu wa muda mrefu Benjamin Netanyahu atabakia madarakani

https://p.dw.com/p/3YiKg
Kombibild: Benny Gantz und Benjamin Netanjahu

Waisrael wanapiga kura leo katika uchaguzi usio wa kawaida na wa tatu nchini humo kuandaliwa katika kipindi cha mwaka mmoja utakaoamua kama Waziri Mkuu wa muda mrefu Benjamin Netanyahu atabakia madarakani licha ya kesi yake inayosubiriwa kuanza kuhusu mashitaka ya ufisadi. 

Netanyahu, kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Israel, amekuwa waziri mkuu wa mpito kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati Israel iliyogawika ikijikuta katika hali ya mkwamo kutokana na chaguzi mbili ambazo zimesababisha mzozo wa kisiasa kutokana na kushindwa kuundwa serikali.

Huku uchunguzi wa maoni ukionyesha mkwamo mwingine, Netanyahu anatafuta uungwaji mkono wa dakika za mwisho kupata wingi wa viti bungeni pamoja na vyama vingine vya siasa za kizalendo ambavyo vitampa muhula wa nne mfululizo madarakani, na wa tano kwa ujumla.

Benny Gantz
Jenerali wa zamani jeshini Gantz anampinga NetanyahuPicha: Reuters/A. Cohen

Anakabiliwa na ushindani mkali kwa mara nyingine kutoka kwa jenerali mstaafu wa jeshi Benny Gantz, ambaye chama chake cha siasa za wastani cha Bluu na Nyeupe au Blue and White, kinapambana kwa nguvu sawa na cha Netanyahu Likud kikituma ujumbe kuwa waziri mkuu huyo wa mda mrefu wa Israel hastahili kuongoza kwa sababu ya mashitaka makubwa dhidi yake.

Israel imeweka vituo 15 kuruhusu upigaji kura wa mamia ya Waisrael walioamrishwa kubaki majumbani mwao baada ya kuwa katika kitisho cha kuambukizwa virusi vya corona.

Mwanasiasa mashuhuri Avigdor Lieberman kwa mara nyingine anaonekana kuwa mpatanishi, kwa sababu Netanyahu au Gantz hatapata wingi wa viti bungeni bila msaada wake. Lieberman hajatangaza anamuunga mkono mgombea yupi, ijapokuwa ameahidi kuwa hakutakuwa na uchaguzi wa nne.

Israel Hadera | Wahlplakat von Benjamin Netanyahu
Netanyahu anakabiliwa na kesi ya rushwaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Schalit

Netanyahu anahitaji kupata ushindi mwembamba wa wingi wa vita 61 katika bunge la Knesset pamoja na washirika wake wa misimamo mikali ya kidini na kizalendo, kabla ya kuanza kesi inayomkabili wiki mbili baadaye. Ameshindwa kupata kinga dhidi ya kesi hiyo, lakini akibakia madarakani huenda akatafuta mbinu nyingine za kuukwamisha mchakato wa kisheria dhidi yake.

Netanyahu anafikishwa mahakamani Machi 17 kwa mashitaka ya rushwa, ulaghai na uvunjifu wa uaminifu kutokana na tuhuma kuwa alikubali zawadi za kifahari kutoka kwa marafiki wake mabilioneya na kuahidi kushinikiza sheria itakayolifaidi gazeti moja kuu nchini humo ili naye apewe umaarufu. Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa moja asubuhi na vitafungwa saa nne kamili usiku. Matokeo rasmi yanatarajiwa usiku wa manane.

Hapo sasa kazi itakuwa kwa Rais Reuven Rivlin ambaye ana jukumula kumteuwa mgombea wa wadhifa wa waziri mkuu. Anapaswa kumteuwa kiongozi ambaye anaamini ana nafasi nzuri Zaidi ya kuunda serikali imara ya muungano.