1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya kudhoofisha muungano wa Scholz?

8 Juni 2024

Uchaguzi unaoendelea wa Bunge la Ulaya unaweza kuwa na matokeo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa Chama cha SPD cha Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na washirika wake wa muungano.

https://p.dw.com/p/4goeL
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Kai Pfaffenbach/Reuters/pool/dpa/picture alliance

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya unatoa kitisho na shinikizo kubwa kwa Kansela Olaf Scholz na washirika wake wa muungano hasa katika mwaka muhimu kwa siasa za Ujerumani. Matokeo hafifu yatakuwa ishara mbaya kwa chama cha Scholz cha SPD takriban miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa majimbo matatu eneo la mashariki, ambapo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala wa Ujerumani (AfD) kinatabiriwa kupata matokeo bora.

Uchaguzi ujao wa kitaifa wa mwaka 2025 pia unakaribia. Uwezekano wa Kansela Scholz kuendelea kushikilia wadhifa wake unaonekana kuwa mdogo mno. Muungano wa Scholz unahitaji nguvu na ari mpya, lakini uchaguzi huu wa Bunge la Ulaya utakaofanyika nchini Ujerumani siku ya Jumapili hautoi matarajio kwa Scholz wala chama chake cha Social Democrats (SPD) au hata serikali yake ya mseto.

Uchaguzi EU 2024 | Makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels
Eneo kwenye Ofisi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels, UbelgijiPicha: Ardan Fuessmann/IMAGO

Mtaalam wa masuala ya kisiasa wa Bremen Lothar Probst, anasema hata kabla ya uchaguzi huu, Kansela Scholz hakuchukuliwa kama mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Umoja wa Ulaya, na matokeo hafifu kwa chama chake yataashiria hatari ya kupoteza zaidi ushawishi wake na hata kupoteza uungwaji mkono ndani ya chama chake.

Soma pia: Nani kuchukua usukani wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya

Kura za maoni kuhusu uchaguzi huu wa Bunge la Ulaya zinaipatia SPD karibu asilimia 14 ya kura, ikiwa ni matokeo ya chini kidogo ukilinganisha na mwaka 2019 ambapo SPD ilijipatia asilimia 15.8. Matokeo yote hayo ni hafifu ukilinganisha na asilimia 25.7 alizojipatia Scholz aliposhinda uchaguzi wa shirikisho mnamo mwaka 2021. Ingawa ushindi huo ulio mdogo, lakini ulifungua njia kwa SPD kurejea madarakani katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya baada ya utawala wa kihafidhina wa miaka 16 wa Kansela Angela Merkel.

Vyama vya muungano wa Scholz mashakani

Berlin | Wanasiasa wa Muungano wa Scholz
Wanasiasa wa Muungano wa Scholz. (Kutoka kushoto) : Omid Nouripour, Olaf Scholz, Christian Lindner na Saskia Esken: 04.09.2022Picha: Frederic Kern/Future Image/IMAGO

Vyama vilivyopo kwenye serikali ya mseto ya Scholz pia vinakabiliwa na changamoto. Chama cha Kijani kinatarajiwa kupata karibu asilimia 13 ya kura ikiwa ni matokeo hafifu ukilinganisha na asilimia 20.5 iliyojipatia katika uchaguzi wa Ulaya mnamo mwaka 2019.

Wakati huohuo, chama cha waliberali cha Free Democrats (FDP), kinakadiriwa kupata asilimia 4 tu. Kwa pamoja, muungano huu unaofahamika zaidi kama "Traffic light" kutokana na rangi nyekundu, kijani na njano ya vyama hivyo unatarajiwa kukusanya jumla ya asilimia 31 ya kura. Ikiwa matokeo haya yataakisi uchaguzi wa wa Bunge la Ujerumani Bundestag basi hii itamaanisha kuwa muungano huo hautoweza kuwa na wingi wa viti bungeni.

Soma pia: Ujerumani na shauku duni ya uchaguzi wa Umoja wa Ulaya

Aidha, raia wengi wa Ujerumani wanaonekana kutoridhishwa na utawala wa Scholz, huku asilimia 59 wakitathmini kazi yake kama kansela kuwa ni "mbaya", hii ikiwa ni kulingana na utafiti wa hivi majuzi. Miaka miwili na nusu ya uongozi wake, kuna sababu mbalimbali zilizopelekea umaarufu wa muungano huu wa mrengo wa kati kupungua.

Bunge la Ujerumani: Bundestag
Kansela Scholz akilihutubia Bunge la Ujerumani: BundestagPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Zaidi ni wasiwasi juu ya kuongezeka kwa wahamiaji na hisia kwamba tawala za manispaa zimetelekezwa katika kushughulikia suala hilo. Mnamo mwaka 2022, uhamiaji nchini Ujerumani ulifikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa hasa kutokana na wimbi la wakimbizi wanaokimbia vita nchini Ukraine.

Suala hilo la uhamiaji, sera ya nishati na mizozano kati ya vyama vya muungano vilisababisha raia kupunguza uungwaji wao mkono kwa utawala wa Scholz lakini pia yote hayo yalitumiwa na vyama vya mrengo wa kulia kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa  raia wa Ujerumani.

(Chanzo: DPAE)