1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu wafanyika Angola

31 Agosti 2012

Nchini Angola, vituo vya kupigia kura vimefunguliwa kwa uchaguzi mkuu ambapo watu wapatao millioni tisa wanatarjiwa kupiga kura. Chama tawala cha MPLA ndicho kinachopewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda.

https://p.dw.com/p/161OH
Raia wa Angola wapiga kura
Raia wa Angola wapiga kuraPicha: DW

Hii ni mara ya tatu kwa uchaguzi mkuu kufanyika Angola tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka kwa watawala wa kikoloni mwaka 1975. Mara ya mwisho, uchaguzi ulifanyika mwaka 2008 na kabla ya hapo mwaka 1992 ambapo matokeo ya uchaguzi yalizua mgogoro ulioitumbukiza Angola katika awamu ya pili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu hadi mwaka 2002. Katika uchaguzi wa mwaka huu, zaidi ya shule na vyuo 10,000 viligeuzwa kuwa vituo vya kupigia kura. Vituo hivyo vilifunguliwa saa moja asubuhi na vitafungwa saa 12 jioni.

Chama tawala cha Ukombozi wa Angola - MPLA, ndicho kinachopewa nafasi kubwa zaidi ya kuushinda uchaguzi wa leo. Rais dos Santos, ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miaka 33 sasa, ataongezewa miaka mingine mitano ya kuiongoza nchi yake. Alipokuwa akitoa hotuba ya kufunga kampeni siku ya Jumatano, dos Santos alionyesha kuwa mwenye kujiamini: "Ujenzi wa nchi yetu unaendelea. Kwa namna hiyo tunachangia vikubwa katika kuboresha hali ya maisha ya raia wa Angola," alisema dos Santos. "Maendeleo yanaletwa na mimi. Upinzani unakosoa tu na kutoa vitisho. Lakini sisi wa MPLA tunafanya kazi kwa ajili ya maslahi ya taifa letu."

Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola
Rais Jose Eduardo dos Santos wa AngolaPicha: Reuters

Upinzani ulitaka uchaguzi uahirishwe

Vyama vya upinzani nchini humo bado havijawa na nguvu ya kuwa kitisho kwa MPLA. Chama kikuu cha upinzani, UNITA, kilipigana vita na utawala hadi pale kiongozi wake Jonas Savimbi alipouliwa na wanajeshi mwaka 2002. Mwenyekiti wa chama hicho, Isaias Samakuva, ameishutumu tume ya uchaguzi kwa kufanya makosa na kuvunja sheria katika kuuandaa uchaguzi wa leo. "Tulitaka uchaguzi uahirishwe. Ni bora kusubiri kwa mwezi mmoja hadi pale ambapo taratibu zote zitafuatwa kulingana na sheria. Lakini hatua hiyo haijachukuliwa," alisema Samakuva.

Mwanamke mmoja akiwa katika kituo cha kupigia kura
Mwanamke mmoja akiwa katika kituo cha kupigia kuraPicha: Reuters

Tume ya uchaguzi ya Angola inatakiwa kutoa matokeo ya uchaguzi katika siku saba zijazo. Hata hivyo, matokeo ya awali yanaweza hata kutolewa mwishoni mwa wiki hii. Zaidi ya waangalizi 97,000 kutoka vyama 9 vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huu watasimamia shughuli zote za upigaji kura.

Angola ni moja ya nchi za Afrika ambazo uchumi wao unakua kwa kasi. Ukuaji huo kwa Angola unatokana na mauzo ya mafuta. Hata hivyo, sehemu kubwa ya vijana hawana ajira na ujenzi wa miundombinu nje ya mji mkuu Luanda, unaendelea kwa kiwango kidogo sana.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman