Ubelgiji: msamaha kwa uetekaji nyara wa watoto machotara
5 Aprili 2019Waziri Mkuu wa Ubeligiji, Charles Michael, aliomba msamaha kwa madhila yaliyofanywa na Wabelgiji kwenye makoloni yao ya Afrika nchini Kongo, pamoja na Rwanda na Burundi.
"Kwa niaba ya serikali kuu, ninaomba msamaha kwa watoto machotara wenye chimbuko la ukoloni wa Ubelgiji na kwa familia zao kwa mateso waliyopitia. Pia ninaomba kueleza masikitiko yetu kwa akinamama wa Kiafrika waliotenganishwa na watototo wao," alisema Michael.
Ombi hilo la msamaha ni la kwanza kabisa kuombwa na Ubelgiji katika harakati za kutambua majukumu ya sera za kibaguzi wakati wa ukoloni ambapo ilikuwa ni kosa kwa ndoa za makabila mchanganyiko na kufanya kuwepo kwa watoto machotara waliozaliwa na mama wa Kikongo na baba wa Kibelgiji kuwa kama uvunjwaji wa sheria hiyo.
Watoto hao walikuwa wakitekwa nyara kutoka Kongo na kupelekwa katika mashule na makaazi ya watoto yatima nchini Ubeligiji yaliyokuwa yakisimamiwa na Kanisa Katoliki.
Bunge lilipitisha azimio la kuomba msamaha
Mwaka uliopita, bunge lililipitisha kwa wingi kura ya azimio kuitaka serikali kuu iombe msamaha na kutambua madhila yaliyofanywa na serikali pamoja na Kanisa Katoliki katika kipindi cha ukoloni wao nchini Burundi, Kongo na Rwanda.
Mmoja wa wahanga wa kutekwa huko, Jeannot Cardinael, alishiriki wakati wa mkutano huo wa waziri mkuu wa Ubelgiji.
"Nimeguswa na nimefurahi sana kwamba baada ya miaka mingi, waziri mkuu ametambua mambo tuliyopitia katika miaka yote hiyo. Huku ni kutambuliwa kwa kitu kilichofaywa na serikali ya Ubelgiji kwetu wakishirikiana na kanisa. Waliuchukuwa utambulisho wetu na sasa wanakubali kosa hilo. Najisikia vizuri sasa," alisema Cardinael.
Utawala wa kikoloni wa Ubeligiji nchini Kongo ulikuwa wa kikatili sana. Kati ya mwaka 1885 na 1908 ambapo nchi hiyo ilikua inaitwa Congo Free State, ilikua ikitawaliwa na Mfalme Leopold wa Pili wa Ubelgiji kama shamba lake binafsi.
Utumwa ulitumika katika kuendeleza kilimo cha mpira na Waafrika waliteswa sana, ambapo watu kati ya milioni 10 mpaka 15 waliuawa.