Uamuzi wa Rais Sall wapokelewa kwa hisia mseto
4 Julai 2023Uamuzi wa Sall kutowania muhula wa tatu wenye utata, ulipokelewa kwa hisia mseto na wafuasi wake nje ya makao makuu ya chama tawala katika viunga vya mji mkuu wa Dakar. Baadhi walibubujikwa na machozi na kukumbatiana, wengine wakikaa kimya wakitafakari tangazo lake. Tangu awali kulikuwa na uvumi kwamba kiongozi huyo angejaribu kuwania muhula mwingine madarakani, lakini kwa maneno yake, muhula wa 2019 ndio ulikuwa wa mwisho kwake kuongoza. "Ningependa kusema kwamba nina akili na kumbukumbu ya wazi ya kile nilichokisema, kuandika na kukirudia hapa na mahali pengine, ambacho ni kwamba muhula wa 2019 ulikuwa ndio muhula wangu wa pili na wa mwisho," alisema Rais Sall.
Kabla ya uamuzi wake, wasiwasi ulikuwa umetanda kwamba rais Sall angeweza kufuata nyendo za viongozi wengine wa kikanda ikiwemo Ivory Coast na Togo ambao walitumia mabadiliko ya Katiba kama kisingizio cha kusalia mamlakani. Mkaazi mmoja wa Dakar na mfuasi wa Rais Sall anaelezea hisia zake: "ni chaguo lake na yeye ni kiongozi wetu. Tunakubali uamuzi wake na tutamuunga mkono yeyote atakayemteua. Lakini angeweza kutawala kwa muhula mwingine wa miaka mitano kwasababu ana kila haki ya kufanya hivyo. Lakini ameamua kufanya hivyo na tunaheshimu utashi wake"Senegal: Utulivu warejea baada ya maandamano yenye ghasia
Mfuasi mmoja wa upinzani nchini humo ambaye ameonekana kuridhishwa na tangazo la Rais Sall alielezea maoni yake kwamba; "tunahitaji rais ambaye anawahurumia Wasenegal. Tunahitaji rais asiyeua watu wake. Tunahitaji rais anayesikiliza watu wake. Raia wa Senegal lazima wajisikie fahari na kuishi sawa kama raia wa Marekani".
Viongozi wa kikanda, wakiwemo marais wa Niger, Mohamed Bazoum, Umaro Sissoco Embalo wa Guinea Bissau, na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat waliusifu uamuzi wa Sall, wakati Bazoum akiongeza kuwa utapunguza hofu. Senegal ilikabiliwa na maandamano makubwa mwezi uliopitaambayo yalichochewa na hukumu ya kiongozi mkuu wa upinzani Ousmane Sonko ya miaka miwili jela kwa mashitaka yanayohusiana na ubakaji, madai ambayo ameyakana na kusema yamechochewa kisiasa ili kumzuia kuwania uchaguzi.
Sonko tayari alikuwa ametoa wito wa maandamano zaidi nchini Senegalkama Sall angeamua kutangaza nia yake ya kugombea tena katika uchaguzi wa mwezi Februari. Sall alichaguliwa rais wa Senegal kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012 kwa muhula wa miaka saba baada ya kumpiku aliyekuwa rais wa wakati huo Abdoulaye Wade,na kisha kuchaguliwa tena 2019 kwa muhula wa pili wa miaka mitano. Na mwaka wa 2016, Sall aliirekebisha Katiba na kuweka ukomo wa mihula miwili ya urais. Wafuasi wake walisisitiza kuwa muhula wake wa kwanza chini ya katiba ya awali usingehesabika.
Vyanzo: Reuters/ap