Tuzo ya Mo Ibrahim 2016 yakosa mshindi
28 Februari 2017Tangazo hilo lilitolewa Jumanne ( Februari 28 ) kutokana na mkutano wa kamati uhuru ya tuzo hiyo, chini ya Uweyekiti wa Dr Salim Ahmed Salim pamoja na mkutano wa bodi ya wakfu huo uliofanyika mwishoni mwa juma lililopita.
Akizungumzia juu ya uamuzi wa kamati ya tuzo hiyo ya Mo Ibrahim, Dr Salim alisema "kama ninavyosisitiza kila mwaka, paliwekwa kipimo cha hali ya juu, wakati tukizindua tuzo hii 2006.
Tunatambua na kupongeza mchango muhimu unaotolewa na viongozi wengi wakiafrika kuleta mabadiliko katika nchi zao. Lakini tuzo hii inakusudiwa kumulika na kusherehekea uongozi wa aina yake, jambo ambalo si la kawaida ukizingatia kielelezo halisi."
Dr Salim akaongeza kusema kwamba baada ya zingatio makini, kamati hiyo imeamua kutomzawadia yeyote tuzo hiyo kwa mwaka 2016.
Wagombea wote wa tuzo ya Ibrahim ni ama viongozi wa taifa au Serikali waliondoka madarakani katika kipindi cha miaka mitatu iliopita na ambao walikuwa wamechaguliwa kidemokrasi na kutumikia vipindi vyao kwa mujibu wa katiba.
Tangu ilipoanzishwa 2006, tuzo ya Mo Ibrahim imeshatolewa mara nne. Washindi waliopita ambao wote walikuwa marais wa nchi zao ni, Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014), Pedro Pires wa visiwa vya Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2008). Rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela alitunukiwa tuzo ya heshima 2007.
Wakfu wa Mo Ibrahim unatarajia kuwa na tamasha maalum la "Wikiendi ya Utawala," mjini Marrakech Morocco kuanzia Aprili 7-9 2017. Tamasha hilo litafunguliwa Ijumaa jioni kwa mjadala wa ngazi ya juu uliopewa jina "Mazungumzo kuhusu Uongozi", yakizingatia changamoto za uongozi duniani katika karne ya 21.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman / Mtandao wa Mo Ibrahim
Mhariri: Iddi Ssessanga