1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo ya amani ya Nobel atunukiwa mpinzani wa serikali ya China

Oumilkher Hamidou8 Oktoba 2010

Mpinzani wa mfumo wa kikomonisti,Liu Xiaobo ametunukiwa zawadi ya amani Nobel kwa juhudi zake za kudai demokrasia nchini mwake

https://p.dw.com/p/PZEb
Mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel mwaka 2010-Liu XiaoboPicha: AP

Tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2010 ametunukiwa mpinzani wa China aliyewekwa korokoroni kwasababu ya juhudi zake za kudai demokrasia Liu Xiaobo.Zaidi anasimulia Oummilkhheir.

Liu, mwenye umri wa miaka 54 anatumikia kifungo cha miaka 11 jela kwa kile kinachodaiwa kuwa "kusaliti taifa",baada ya kuwa miongoni mwa waasisi wenza wa "waraka wa 2008" unaodai pawepo mfumo wa kidemokrasi nchini China.

Harakati zake za kisiasa zimemsababishia kifungo kwa muda wa miaka kadhaa.

Mwaka 1989 aliporejea nyumbani kutoka Marekani ambako alikuwa akisomesha katika chuo kikuu cha Columbia University mjini New-York alishiriki katika vurugu vugu la wanafunzi wapenda demokrasia katika uwanja wa Tiananmen.

Kutokana na ushupavu wa serikali Liu alianzisha mgomo wa kutokula chakula katika uwanja huo mashuhuri mjini Beijing akishirikiana na muimbaji Hou Dejian na wasomi wenzake wawili Zhou Duo na gao Xin.

"Bora tuwe na mafirauni kumi kuliko malaika mmoja anaedhibiti madaraka peke yake"-waliandika katika waraka wao uliochapishwa hadharani.Hiyo ilikuwa katika mwaka 1989,kabla ya jeshi kuingilia kati na kuwatawanya kwa nguvu waandamanaji katika uwanja wa Tiananmen.

Katika kuadhimisha miaka 60 ya azimio la haki za binaadam,Liu alikua miongoni mwa waasisi wa "waraka wa 2008-" unaotoa mwito wa kuheshimiwa haki za binaadam na uhuru wa mtu kutoa maoni yake pamoja na kuanzishwa uchaguzi huru kwaajili ya taifa huru na la kidemokrasia.

Harakati hizo zikapelekea ahukumiwe kifungo cha miaka 11 jela,X-Mas mwaka jana.Hukmu hiyo imedhibitishwa pia na korti ya rufaa.

Liu Xia / Frau von Liu Xiaobo / China
Liu Xia, mke wa mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel Liu XiaoboPicha: AP

Mkewe Liu Xia amefurahishwa na uamuzi wa kumtunukia mumewe zawadi ya amani ya Nobel na anasema:

"Wengi waangekua wameshasalim amri.Lakini Xiaobo mkaidi kweli kweli.Akidhamiria kitu mpaka akikamilishe hata kama anatambua fika kamwe hatofanikiwa.Mkaidi kweli kweli."

Katika mahojiano aliyofanya mwaka jana Liu Xiaobo amesema hata hivyo ana matumaini makubwa."Mambo yanaendelea kidogo kidogo,madai ya uhuru kutoka kwa wananchi wa kawaida pamoja pia na wanachama wa chama tawala-hayazuwiliki."

Kwa maoni ya Liu Xiaobo ambae hakani maendeleo yaliyoweza kupatikana tangu mwaka 1989,chama cha kikoministi kitalazimika kujirekebisha kutokana na shinikizo la umma uliochoshwa na kuambiwa uwongo.

Itafaa kusema hapa kwamba wasomi,waandishi vitabu na mawakili zaidi ya 120-wengi wao wakiwa wa kutoka China walitoa mwito kupitia mtandao wa Internet kutaka tuzo ya amani ya mwaka huu atunukiwe yeye Liu Xiaobo.Mwito wao umeitikwa.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ afp/reuters

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman