1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunakuunga mkono Rais wa Liberia! asema Clinton

Thelma Mwadzaya14 Agosti 2009

Marekani imetangaza kuwa inamuunga mkono Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf anayekabiliwa na shinikizo za kujiuzulu.Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton.

https://p.dw.com/p/J9Ok
Waziri wa mambo ya nje wa marekani Hillary Clinton akikamilisha ziara ya AfrikaPicha: AP / DW Montage

Marekani imetangaza kuwa inamuunga mkono Rais wa Liberia Ellen Johnson-Sirleaf aliye kiongozi wa kike pekee wa ngazi hiyo barani Afrika.Kauli hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton aliye katika kituo chake cha sita cha ziara ya bara la Afrika.

Kulingana na Bibi Clinton Marekani imefurahishwa na hatua zilizopigwa na Liberia chini ya uongozi wa Rais Ellen –Johnson Sirleaf.Bibi Clinton alisisitiza kuwa Liberia iko katika mkondo wa sawa na Marekani itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Ellen Johnson-Sirleaf Präsidentin Liberia
Rais wa Liberia Ellen Johnson-SirleafPicha: picture-alliance / s65 / ZUMA Press

Rais Sirleaf anashinikizwa kujiuzulu baada ya Tume ya kitaifa ya Ukweli na Maridhiano kupendekeza apigwe marufuku kushiriki katika siasa nchini humo kufuatia madai ya kushirikiana na wababe wa kivita wakati Liberia ilipokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.Bibi Sirleaf kwa upande wake ameyakanusha madai hayo.Hillary Clinton anatarajiwa kuihitimisha ziara yake ya siku 11 barani Afrika kisiwani Cape Verde hii leo.