1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Tanzania yamuita Tundu Lissu

George Njogopa28 Septemba 2020

Tume ya Uchaguzi Tanzania imemtaka mgombea wa chama cha upinzani Chadema, Tundu Lissu kujitokeza katika kamati ya maadili ya tume hiyo kujibu baadhi ya hoja alizoziibua kwenye kampeni.

https://p.dw.com/p/3j5uy
Tansania Wahlkampagne Tundu Lissu, Kandidat der Opposition
Picha: Getty Images/AFP

Tundu Lissu ametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo siku ya Jumanne.

Mgombea huyo ambaye yungali akizunguka kwenye mikutano yake ya kampeni katika kanda ya ziwa, ameshutumia kutumia lugha zisizostahili dhidi ya mgombea wa chama tawala pamoja na tume yenyewe ya uchaguzi.

Kulingana na mkurugenzi wa tume hiyo, Dr Wilson Mahera mgombea huyo anapaswa kufika katika kamati ya maadili Septemba 29, kujibu hoja kadhaa alizoziibua wakati akihutubia katika mikutano yake ya kampeni.

Soma pia: Wagombea Tanzania walalamikia uhalifu kwenye kampeni

Kulingana na mwongozo wa tume hiyo, iwapo Lissu atatiwa hatiana anaweza kukumbwa na adhabu ya kusimamishwa kufanya kampeni kwa kipindi kinachoanzia siku saba.

Tume hiyo imesisitiza kwamba, ingawa imekuwa ikikumbana na changamoto za hapa na pale, inaendesha mambo yake kwa kufuata sheria na kutenda haki.
Tume hiyo imesisitiza kwamba, ingawa imekuwa ikikumbana na changamoto za hapa na pale, inaendesha mambo yake kwa kufuata sheria na kutenda haki.Picha: DW

Hadi sasa hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa na mgombea huyu Tundu Lissu wala chama chake kuhusiana na hatua hiyo ya tume, ingawa baadhi ya duru za habari zimenukuu akaunti ya twitter ya Lissu aliyesema anaendelea na kampeni zake kama kawaida.

Mbali ya hatua hiyo ya tume, Lissu amesema chama chake kimetakiwa kutoa maelezo na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuhusiana na yale yanayoendelea kwenye kampeni zake.

Suala la utendaji wa tume ya uchaguzi imekuwa ni mada inayojitokeza mara kwa mara wakati na hata baada ya uchaguzi huku sehemu kubwa ya vyama vya upinzani vikisisitiza kuundwa kwa tume huru.