1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai sasa waziri mkuu

Kalyango Siraj15 Septemba 2008

Mugabe azishambulia Marekani na Uingereza

https://p.dw.com/p/FIlC
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, katikati, pamoja na waziri mkuu wake mpya , Morgan Tsvangirai, kushoto na naibu waziri mkuu Arthur Mutambara, kulia.Picha: AP

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe Morgen Tsvangirai ameteuliwa kuwa waziri mkuu katika serikali inayoongozwa na mpinzani wake mkuu kisiasa rais Robert Mugabe.

Hatua hii imechukuliwa jumatatu baada ya viongozi hao wawili kutia sahihi mkataba wa kugawana madaraka katika sherehe iliofanyika mjini Harare.

Kuteuliwa kwa Tsvangirai kama waziri mkuu kunafuatia majadiliano makali yaliyodumu majuma matatu yaliyokuwa na nia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa ulioikumba nchi ya Zimbabwe kwa mda.Mgogoro unafuatia kuchaguliwa tena kwa rais Mugabe katika uchaguzi mkuu wa juni mwaka huu ambao unasemekana kuwa wa utata na pia kulaaniwa na viongozi kadhaa wa nchi za magharibi.

Baada ya sherehe ya kutia saini mkataba huo rais Mugabe ameonyesha wazi kuwa hajatetereka katika hatua yake ya kuyashambulia mataifa ya kimagharibi hususan mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Uingereza.Amesema kuwa Uingereza inataka kuendelea

kuidhibiti Zimbabwe,licha ya kuwa taifa hilo ni huru.

Mpatanishi mkuu wa mgogoro huo na aliefanikisha makubaliano hayo rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini amenukuliwa kusema kuwa pande zote mbili hazijakubaliana kuhusu mawaziri wangapi watakaojumulishwa katika serikali ya muungano.

Lakini suala la mawaziri wangapi watakaounda serikali yakiwekwa kando yeye waziri mkuu mpya Morgen Tsvangirai baada ya sherehe ya kutia saini alisema njia wanazo kwa sasa.Miongoni mwa njia hizo ni aidha kuacha tofauti zao na badala yake wakazanie kuiendeleza nchi ama kuendeleza mkwamo na hivyo kuitatiza Zimbabwe.Ameongeza kuwa yeye kwa upande wake mstakabala wa Zimbabwe ni muhimu mno kuliko matatizo aliyopitia

Miongoni mwa mateso ya wakati uliopita ni kugawanyika kwa chama chake cha MDC.Mmoja wa wanachama wake Arthur Mutambara aliunda tawi lake, nae katika makubaliano amekuwa naibu wake.Huku raia wa Zimbabwe wakisherehekea hatua iliofikiwa mjini Harare alitoa onyo dhidi ya changamoto zinazowakabili .Amesema miongoni mwa hizo ni kuwaunganisha mahasimu wa zamani katika jukumu la kuendeleza Zimbabwe

Mataifa ya magharibi yana hamu ya kujua yaliyomo katika makubaliano hayo na jinsi yatakavyo tekeleza. Hata hivyo umoja wa Ulaya umesema jumatatu kuwa uko tayari kuisaidia Zimbabwe ikiwa serikali mpya itachukua hatua za kurejesha demokrasia pamoja na utawala wa sheria.