1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai akubali kushiriki katika serikali ya mseto Zimbabwe

Aboubakary Jumaa Liongo28 Januari 2009

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha MDC, Morgan Tsvangirai, amesema kuwa amekubali kushiriki katika kuundwa serikali ya kitaifa nchini humo.

https://p.dw.com/p/Ghn9
Kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai,Picha: AP

Kwa mujibu wa Gazeti moja la Afrika Kusini, Tsvangirai amesema hayo siku moja tu baada ya chama hicho cha MDC kukataa makubaliano yaliyofikiwa na wakuu wa nchi za SADC juu ya suala la mkwamo wa kisiasa nchini Zimbabwe.


Akinukuliwa na gezeti hilo la Afrika Kusini liitwalo star, Morgan Tsvangirai amesema kuwa kazi ya kuondoa vikwazo vilivyomo katika utekelezaji wa makubaliano ya kuundwa serikali hiyo ya kitaifa inafanyika na kwamba, kimsingi, amekubalia kuundwa kwa serikali hiyo.


Hapo jana wakuu hao wa nchi za SADC, katika mkutano wao wa siku mbili nchini Afrika Kusini, waliamua ya kwamba Zimbabwe ni lazima iunde serikali ya Umoja wa kitaifa ifikapo mwezi ujayo, lakini chama cha MDC kilitoa taarifa kikisema kuwa kimekatishwa tamaa na maamuzi hayo, na hivyo kupelekea wasi wasi wa kumalizika kwa mkwamo huo.


Chama hicho kilisema kuwa baraza la chama hicho litakutana kutathmini nafasi yake kwenye maamuzi hayo ya wakuu wa SADC.


Kauli ya Tsvangirai inaashiria mgawanyiko katika chama hicho kuhusiana na utekelezaji wa mkataba wa kugawana madaraka uliyotiwa saini mwezi Septemba mwaka jana.


Hatua hiyo inatia shaka kama iwapo serikali hiyo mpya itakayoundwa itakuwa katika nafasi ya kupambana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo kwa sasa.


Rais Robert Mugabe ambaye aliweka wazi kuwa ataunda serikali punde baada ya mkutano huo wa wakuu wa SADC, hata ikibidi bila ya upinzani, amesema kuwa mazungumzo yamekamilika na kwamba baraza la mawaziri litaundwa hivi karibuni.


Kwa mujibu wa Rais Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini, wakuu hao wametaka kutekelezwa haraka kwa makubalino ya kugawana madaraka.


Morgan Tsvangirai ambaye chini ya makubaliano hayo ya Septemba anakuwa Waziri Mkuu wa Zimbabwe amesema kuwa kila mtu anakubali kwamba tatizo lililopo ni kuondoa baadhi ya vikwazo katika utekelezaji wa makubaliano hayo, kwa hivyo kimsingi serikali ya mseto inaweza ikaundwa.


Kwa mantiki hiyo, amesema kuwa anakubaliana na kuundwa kwa serikali hiyo ya kitaifa, hatua ambayo inategemewa kusaidia kuinasua Zimbabwe kutoka katika matope ya kuanguka kwa uchumi.


Mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo wamelazimika kukimbilia katika nchi jirani kutafuta kazi kutokana na hali mbaya ya uchumi, ambayo imeshuhudia mfumuko mkubwa kabisa wa bei kuwahi kuhushuhudiwa.


Aidha zaidi ya watu elfu tatu wamekufa kutokana na mripuko wa maradhi ya kipindupindu.Tayari watu elfu 56 wanaripotiwa kuathiriwa na maradhi hayo.


Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO, linasema kuwa mripuko wa maradhi hayo ni mbaya kabisa kuwahi kuikumba nchi yoyote Barani Afrika.