Tshisekedi akikosoa kikosi cha kikanda
10 Mei 2023Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi jana amekikosoa kikosi cha jeshi cha kanda kilichopelekwa na mataifa ya Afrika Mashariki kurejesha utulivu mashariki mwa nchi hiyo, na kudokeza kuwa wanajeshi hao wanaweza kuondoka kufikia mwishoni mwa Juni. Akizungumza wakati wa ziara nchini Botswana, Tshisekedi alielezea wasiwasi kuhusu usuhuba kati ya waasi na kikosi hicho kilichoanza kupelekwa huko mwishoni mwa mwaka jana. Mataifa saba wanachama wa EAC yaliunda kikosi cha jeshi kuingilia kati mzozo wa mashariki mwa Kongo Juni mwaka jana, ambapo wanajeshi wa Kenya walikuwa wa kwanza kupelekwa mwezi Novemba na kufuatiwa mwaka huu na vikosi kutoka Burundi, Uganda na Sudan Kusin. Tshisekedi alisema kwenye mkutano na waandishi habari kwamba wamebaini kuwepo na ushirikiano kati ya kikosi cha EAC na waasi.