Trump na Biden wapelekana bega kwa bega
4 Novemba 2020Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Biden ameshinda kwenye majimbo ya Virginia, Delaware,Vermont Connecticut, Illinois, Maryland, Massachusetts, New Jersey na Rhode Island huku Trump akiyanyakua majimbo la Virginia magharibi, Kentucky, na South Carolina, Alabama, Mississippi, Oklahoma na Tennessee.
Mpaka sasa Joe Biden anaongoza kwa kura za wajumbe maalum 131 na Trump akiwa na idadi ya kura 98 za wajumbe maalum. Matokeo yanaendelea kutangazwa.
Wamarekani zaidi ya milioni Mia moja wamepiga kura ya kuamua iwapo watamrudisha madarakani Donald Trump au wataamua kuleta mabadiliko kwa kumchagua mgombea wa chama cha Demokratik Joe Biden, baada ya wanasiasa hao wawili kupambana vikali kwenye kampeni zao katika muktadha wa janga la maambukizi ya virusi vya corona.
Idadi hiyo inaashiria kwamba ushiriki wa wapiga kura utavunja rekodi ya karne. Washindani hao walikamilisha kampeni zao kwenye majimbo muhimu. Kura za maoni zinaonyesha kuwa Biden yuko mbele lakini kinyang'anyiro kinakwenda bega kwa bega katika majimbo yanayoweza kuamua mshindi.
Majimbo ya Pennsylvania, Florida na Ohio kuamua mshindi
Macho yote yanaangazia majimbo muhimu kama Pennsylvania, Florida na Ohio.
Rais Trump amekwenda kwenye makao makuu ya kampeni zake katika mji wa Arlington, kwenye jimbo la Virginia kuwashukuru wanakikosi wa kampeni yake. Amewaambia wafuasi wake kuwa usiku wa leo unaweza kuwa mzuri sana. Hata hivyo ametahadharisha kwamba kinachoendelea ni siasa na uchaguzi na kwamba mtu hawezi kuwa na uhakika kabisa.
Mshindani wake Joe Biden amewaambia wanaomuunga mkono kwamba anaweka mbele matumaini badala ya hofu, ukweli badala ya uongo na hoja za sayansi badala ya hadithi. Akihutubia kwenye jimbo lake la uzawa Delaware Biden alisema kuwa anayo matumaini kutokana na idadi kubwa ya vijana na wanawake waliojitokeza kupiga kura.
Ili kuibuka mshindi mgombea anapaswa kupata kura zisizopungua 270 za wajumbe maalumu, Kila jimbo maalumu lina idadi ya kura kulingana na idadi yake ya watu na kwa jumla ziko kura 538. Katika uchaguzi wa safari hii kampeni ziligubikwa na suala la janga la maambukizi ya corona.
Mpaka sasa wamarekani zaidi ya laki 2 na 33 alfu wameshakufa kutokana na maambukizi ya virusi hivyo na wengine wanaokaribia milioni 10 wameambukizwa huku maambukizi yakiongezeka kila siku.
Hata hivyo rais Trump ameendelea kulipuuza janga hilo. Mshindani wake Joe Biden amemlaumu rais huyo kwa kusababisha vifo ambavyo vingeliweza kuepukika. Masuala mengine yaliyozingatiwa katika kampeni za uchaguzi ni juu ya uchumi, ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi.