Trump: ''Marekani Kwanza'' haimaanishi kujitenga
26 Januari 2018Akizungumza leo katika hotuba ya kulifunga Kongamano la Kiuchumi Duniani, mjini Davos, Uswisi, Trump amesema tabia ya kuwanyonya wengine imekuwa ikiharibu masoko na kwamba Marekani haiwezi kulifumbia tena macho suala la biashara isiyo ya haki. Trump aliyekuwa akizungumza mbele ya viongozi wa kisiasa duniani, wataalamu wa benki na wakurugenzi wakuu wa mashirika ya kibiashara, amesema hawawezi kuwa na biashara huru na ya wazi, kama baadhi ya nchi zitaunyonya mfumo huo dhidi ya wengine.
Trump amesema sera yake ya ''Marekani Kwanza'' haina maana ya kujitenga na ametoa wito wa kuwepo ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo nishati, biashara na usalama. Tangu Trump alipoingia madarakani, washirika wa Marekani ikiwemo Ujerumani, wameonya kuhusu sera hiyo ya kujitenga. Onyo kama hilo limetolewa pia na viongozi wengine waliozungumza katika kongamano hilo.
Aonyesha ushirikiano
Aidha, Trump ambaye ameonyesha urafiki na ushirikiano kwa dunia, amesema mwaka wake wa kwanza madarakani ulikuwa wa mafanikio makubwa na kwamba ni muda muafaka wa kuwekeza nchini Marekani. Amesema Marekani huenda ikarejea katika mazungumzo ya biashara huria na mataifa ya Pasifiki. Mapema wiki hii mataifa hayo 11 yalikamilisha mpango wake wa biashara katika ukanda huo bila ya Marekani, baada ya serikali ya Trump kujiondoa katika mazungumzo ya mkataba wa biashara huria katika eneo la Bahari ya Pasifiki, TPP.
Ama kwa upande mwingine, Trump amesema kwamba muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani yameyakomboa kwa karibu asilimia 100 maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS nchini Iraq na Syria na ametoa wito wa kuwepo ushirikiano mkubwa katika kupambana na ugaidi. Pia ameyataka mataifa kuendelea kuishinikiza Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia, huku akirejea wito wake kwa nchi nyingine kuchangia kwa kuzingatia haki katika kuelekea kwenye ulinzi wa kimataifa.
''Tunafanya pia uwekezaji wa kihistoria katika jeshi la Marekani kwa sababu hatuwezi kuwa na mafanikio kama hakuna usalama. Ili kuufanya ulimwengu sehemu salama bila ya kuwepo ugaidi, tunawaomba marafiki na washirika wetu kuwekeza katika ulinzi wao wenyewe na kutimiza majukumu yao kifedha,'' alisema Trump.
Atuma salamu kwa viongozi wa Afrika
Wakati huo huo, Trump amemuomba mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais Paul Kagame kufikisha salamu zake kwa viongozi wengine wa bara hilo wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Trump leo alikutana na Kagame ambaye ni rais wa Rwanda pembezoni mwa Kongamano la Kiuchumi Duniani mjini Davos, ambako baadhi ya viongozi wa kibiashara barani Afrika walisema wanapanga kususia hotuba ya Trump baada ya kuzusha hasira kutokana na matamshi yake kwamba mataifa ya Afrika yananuka uvundo.
Trump amempongeza Kagame kwa kuchukua kijiti cha mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wenye mataifa 55, akisema kuwa hiyo ni heshima kubwa. Umoja huo umemtaka Trump aombe radhi, ingawa kiongozi huyo wa Marekani amekana kutoa matamshi hayo kama ilivyoelezwa na wabunge wa Marekani ambao walihudhuria mkutano wake.
Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, AFP, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf