Trump, Biden kwenye mdahalo mwengine usio rasmi
16 Oktoba 2020Katika kile kinachoonekana kama mdahalo baina yao, vituo viwili hasimu vya NBC na ABC nchini Marekani viliwaalika wagombea hao mahasimu pia kwa wakati mmoja kwa mahojiano ambayo yalirushwa moja kwa moja na kwa wakati mmoja usiku wa Alkhamis (Oktoba 15).
Kwa wengi, mahojiano hayo yamechukuliwa kama duru ya pili ya mdahalo wa uso kwa macho kati ya Trump na Biden, ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika jana, lakini Trump akajitowa baada ya waandaaji kuamuwa ufanyike kupitia mtandao, kufuatia Trump kuuguwa COVID-19 wiki mbili zilizopita. Soma pia: Trump arejea kwenye kampeni baada ya kupona COVID-19
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha ABC mjini Philadelphia, Biden alisema Trump hajayachukulia maradhi hayo, yashayoangamiza Wamarekani zaidi ya 217,000, kwa umakini zaidi.
"Maneno ya rais yana uzito mkubwa, ama yakiwa mazuri au mabaya. Na pale rais anapokuwa havai barakowa ama anawafanyia dhihaka watu kama miye ambao tunavaa barakowa muda mrefu, utaona watu wanasema kwamba kumbe barakowa sio muhimu kiasi hicho," alisema mgombea huyo wa Democratic ambaye anaongoza kwenye kura za maoni.
Trump na makundi ya siasa kali
Suali ambalo lilimfanya Trump kuonesha kukereka zaidi na mtangazaji wa kituo cha ABC mjini Miami ni lile la kuyakingia kifua makundi ya siasa kali na yenye nadharia za upotoshaji, kama vuguvugu la QAnon, ambalo linadai kuwa Trump anapigana vita vya chini kwa chini dhidi ya kundi la waliberali wabakaji watoto wanaoabudu mashetani.
"Silijui. Hapana, silijui. Wewe ndiye unayeniambia kuhusu hilo kundi. Lakini nikwambie kile ninachosikia kuhusu kundi hilo ni kwamba wanapingana kwelikweli na wabakaji watoto wadogo na mimi nakubaliana na msimamo wao huo," Trump alimwambia mtangazaji wa ABC.
Wafuatiliaji wanasema mahojiano hayo yamemuonesha Biden akitowa majibu ya ufafanuzi na ya uchambuzi, huku Trump akitoa matamshi ya ukali na wakati mwengine utetezi usiozingatia ukweli. Shirika la habari la AP limeorodhesha zaidi ya masuala kumi ambayo linasema Trump amedanganya.
Kwa upande mwengine, mahojiano hayo yamethibitisha jinsi kampeni za mwaka huu zilivyoathiriwa pakubwa na janga la virusi vya corona, ambalo limewalazimisha zaidi ya watu milioni 18 kupiga kura zao zaidi ya wiki mbili kabla ya tarehe ya uchaguzi hapo Novemba 3.
Mdahalo wa mwisho baina ya Trump na Biden umepangwa kufanyika tarehe 22 Oktoba mjini Nashville, Tennessee