Trump azionya Urusi na Korea kaskazini
6 Julai 2017Hata hivyo katika mkutano na waandishi habari pamoja na rais wa Poalnd Duda alishindwa kuishutumu moja kwa moja Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani. Sekione Kitojo na taarifa zaidi.
Akitiwa shime na kundi kubwa lenye hamasa nchini Poland likiimba jina lake, Trump aliamua kuonesha kwamba hazifumbii macho hatua za Urusi ambazo zimezusha heka heka kubwa duniani, hususan kutoka kwa mataifa jirani ya mashariki na na eneo la kati barani Ulaya. Ameonya kwamba maslahi ya mataifa ya magharibi yanaingia majaribuni kwa propaganda , uhalifu wa kifedha na vita vya mtandaoni," na kuilazimisha jumuiya ya NATO kujibadilisha.
"Tunaitaka Urusi kusitisha vitendo vyake vya kuyumbisha nchini Ukraine na kwingineko, na kuunga mkono serikali korofi ikiwa ni pamoja na Syria na Iran, na kujiunga na jumuiya ya mataifa yanayowajibika katika mapambano yetu na adui wetu wa pamoja na kulinda ustaarabu wenyewe," Trump alisema katika hotuba katika eneo la uwanja wa Krasinski mjini Warsaw.
Trump ahoji ukweli wa vyombo vya ujasusi
Ni ukosoaji ambao rais huyo hakuonekana kuuelekeza kwa vitendo vya Urusi mwaka jana wakati wa kampeni yake ya urais. Katika mkutano na waandishi habari kabla ya hotuba yake, Trump alihoji ukweli wa vyombo vya kijasusi vya Marekani juu ya kuingiliwa na mataifa ya kigeni katika uchaguzi wa Marekani, akidai kwamba Urusi haikuwa nchi pekee ambayo huenda iliingilia uchaguzi huo. Akizungumza katika mkutano na waandishi habari pamoja na rais wa Poland Andzej Duda , Trump alisema.
"Nadhani ni Urusi , na nadhani inawezekana kuwa watu wengine katika nchi nyingine. Inawezekana kuwa ni watu wengi waliingilia. Nilisema kwa urahisi sana, nafikiri inaweza kuwa ni Urusi, lakini nafikiri inaweza kuwa mataifa mengine na siwezi kunyoosha kidole moja kwa moja, lakini nafikiri watu wengi waliingilia. Nafikiri imetokea kwa muda mrefu, ilikuwa inatokea kwa miaka mingi , mingi sana."
"Hakuna mtu kwa kweli anayefahamu kwa uhakika," amesema Trump.
Akianza ziara yake ya pili nje ya nchi akiwa rais, Trump pia aliionya Korea kaskazini kwamba anafikiria "kufanya vitu fulani vizito" kujibu hatua ya taifa hilo lililotengwa kufanya majaribio ya makombora ambayo yana uwezo wa kufika Marekani licha ya kwamba alikataa kutoa maelezo maalum kuhusu hilo. Trump aliyataka mataifa duniani kote kupambana na tabia mbaya ya Korea kaskazini.
Pia alitangaza bila kusita kwamba Marekani inasimama nyuma ya kifungu namba 5 cha katiba ya NATO kinachohitaji Marekani kuyalinda mataifa mengine wanachama iwapo moja litashambuliwa. Katika ziara yake ya kwanza barani Ulaya kama rais wa marekani mwezi Mei , Trump alikataa kudhibitisha hitaji hilo.
Trump na Putin wanatarajiwa kukutana kesho Ijumaa mjini Hamburg, Ujerumani , pembezoni mwa mkutano wa kilele wa kimataifa wa G20.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe
Mhariri: Idd Ssessanga