1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump awatuma Wanajeshi 5,200 kuilinda mipaka

Caro Robi
30 Oktoba 2018

Marekani imesema inawatuma wanajeshi 5,200 kusaidia kulinda mipaka kati ya nchi hiyo na Mexico, baada ya maelfu ya wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati kujiunga na msafara wa wahamiaji wanaopania kufika Marekani.

https://p.dw.com/p/37MOl
Migranten aus Mittelamerika auf dem Weg in die USA - an der Grenze zu Mexiko
Picha: Reuters/C. Garcia Rawlins

Idadi hiyo ya wanajeshi wanaotumwa kuulinda mpaka ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa huku Rais Donald Trump akizidi kuwa na misimamo mikali kuhusu uhamiaji kuelekea chaguzi za kati kati ya muhula zinazotarajiwa tarehe 6 mwezi ujao wa Novemba.

Jenerali Terrrence O' Shaughnessy, anayesimamia kambi ya wanajeshi walioko Kaskazini mwa Marekani amesema wanajeshi 800 tayari wako njiani kueleka katika mpaka wa Texas na wengine wanaelekea katika mipaka ya California na Arizona. O'Shaugnessy amesema Rais Trump ameweka wazi kuwa ulinzi wa mipaka ni jambo la usalama wa kitaifa.

Huku hayo yakijiri, mamia ya wahamiaji kutoka Honduras wamevuka mto kuingia Mexico, hilo likiwa kundi jipya la wahamiaji wanaoelekea Marekani. Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya wahamiaji 7,000 wako njiani kuelekea Marekani.

Trump ana msimamo mkali kuhusu wahamiaji

Katika kampeini za uchaguzi wa rais mwaka 2016, Trump alitumia suala la uhamiaji haramu kama mojawapo ya ahadi atakazozipa kipaumbele akiingia madarakani, na sasa anatumia suala la msafara wa wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati kukipigia debe chake cha Republican katika uchaguzi wa kati kati ya muhula.

Mexiko - Migranten aus Mittelamerika auf dem Weg in die USA
Maelfu ya wahamiaji kutoka Amerika ya Kati wanaoelekea MarekaniPicha: Getty Images/AFP/G. Arias

Kiongozi huyo wa Marekani amesema wataweka mahema kuwahifadhi wahamiaji wanaotafuta hifadhi badala ya kuwaachia huru wakati kesi zao zinaposikilizwa kwani hivyo wahamiaji zaidi watavunjika moyo kujaribu kwenda Marekani na mahamana  na kuongeza kuwa wataanzisha kile alichokitaja miji ya mahema kila sehemu badala ya kujenga nyumba ambazo zinagharimuu mamilioni ya dola.

Kulingana na utafiti wa maoni ya wapiga kura ulioendesha na taasisi ya utafiti ya Pew kati ya mwezi Septemba na Oktoba, asilimia 75 ya wapiga kura Warublican wamesema uhamiaji haramu ni tatizo kubwa ikilinganishwa na asilimia 19 ya wapiga kura Wademocrats.

Kevin McAleenan, kamishna wa forodha na ulinzi wa mipaka wa Marekani amesmeam kundi la takriban wahamiaji ,500 wanasafiri kupitia kusini mwa Mexico kuelekea Marekani na kunidi jingine la wahamiaji wasiopungua 3,000 wako katika mpaka kati ya Guatemala na Mexico.

Katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, maafisa mapakani wamerekodi kiasi ya watu 1,900 kila siku wakivuka mpaka kwa njia haramu au kujisalimisha huku zaidi ya nusu ya idadi hiyo ikiwa watoto wasioandamana na watu wazima au wazazi na watoto wao.

 

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Grace Patricia Kabogo