Trump awatisha wanaolaani kifo cha Floyd
29 Mei 2020Rais Donald Trump ambaye jana Alhamisi alisema amehuzunishwa na kifo cha George Floyd, mwanaume mweusi aliyofariki dunia akiwa chini ya mikono ya polisi ametoa matamshi hayo ya kitisho baada ya waandamanaji wenye hasira kukichoma moto kituo cha polisi mjini Minneapolis.
Akiandika kupitia ukurasa wa Twitter Trump amesema vurugu zinazoendelea zinafanywa na makundi ya vibaka na zinaharibu heshima anayostahili Floyd aliyefariki dunia siku ya Jumatatu baada ya kukandamizwa shingoni kwa kutumia goti na polisi mmoja mzungu.
Kiongozi huyo aliyeuita mkasa wa Floyd kuwa wakusikitisha amesema tayari amezungumza kwa njia ya siku na Gavana Tim Walz wa Minnesota uliko mji wa Minneapolis na kumuarifu kuwa jeshi liko tayari na litachukua udhibiti pindi waandamanaji wataanza tena kufanya uharibifu wa mali.
Trump ambaye mara nyingi amekuwa kimya linapokuja suala la ukatili wa watu weupe dhidi ya jamii ya wachache ya watu weusi nchini Marekani, amekosoa mwenendo wa polisi aliyesababisha kifo cha Floyd na kutoa wito wa haki kutendeka.
Uchunguzii unafanyika kuhusu kifo cha Floyd
Tayari ofisi ya mwanasheria mkuu na idara ya upelelezi wa jinai mjini Minneapolis imesema inafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kifo cha Floyd ikiwa ni pamoja na jinsi haki za kiraia za mwanaume huo zilivyohujumiwa.
Hapo jana waandamanaji wenye hasira walikichoma moto kituo cha polisi kilichotelekezwa wakati maandamano yaliyoingia siku ya tatu kulaani kifo cha Floyd yakigeuka vurugu na kuenea hadi mji jirani wa St.Paul.
Msemaji wa polisi amethibitisha maafisa wa jeshi hilo kuondolewa kutoka kituo hicho kwa ajili ya ulinzi kabla ya baadaye kuvamiwa na makundi ya waandamaji na kukitia moto.
Maandamano yasambaa miji mingine
Maandamano yalizuka siku ya Jumanne, siku moja baada ya kifo cha Floyd ambaye kupitia video iliyorikodiwa na mpita njia alionekana akiomba msaada kwa kusema anashindwa kupumua wakati polisi mweupe akimkandamiza shingoni kwa kutumia goti akiwa amefungwa pingu.
Floyd ambaye hakuwa na silaha lakini akituhumiwa kutaka kutumia fedha bandia kwenye mgahawa mmoja , alichukuliwa na gari ya wagonjwa kutoka eneo la mkasa huo na baadaye kufariki dunia.
Kifo Floyd kimeutikisa mji wa Minneapolis na kuzusha maandamano kwenye miji mingine kote nchini Marekani huku viongozi wa majimbo wakitoa wito kwa waandamanaji kuacha vurugu.
Mapema jana biashara kadhaa kwenye eneo hilo zililazimika kuwekewa ulinzi zaidi katika juhudi za kuzuia uporaji huku usafiri wa treni za katikati ya mji ukisitishwa kutoka na wasiwasi wa usalama.
Maandamano ya kulaani kifo hicho yameripotiwa tangu mjini New York, Denver, Columbus na hata huko Kentucky.