1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushuru wa asilimia tano kwa bidhaa za Mexico kuanzia Juni 10

Faiz Musa31 Mei 2019

Rais wa Marekani Donald Trump, ametangaza ushuru wa asilimia tano katika bidhaa zote zinazoingia Marekani kutoka nchini Mexico kuanzia Juni 10 ili kuongeza msukumo kwa taifa hilo kuzuia ongezeko la wahamiaji haramu

https://p.dw.com/p/3JXSa
USA verkündet Ende der Strafzölle auf Stahl und Aluminium
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Trump alitangaza kwamba ushuru huo unaweza ukaongezeka hadi asilimia 25 hadi pale tatizo la wahamiaji litakapodhibitiwa. Uamuzi huo ulionyesha kuwa Marekani imefika katika hatua mpya ya kuishinikiza Mexico kuchukua hatua kwa wakimbizi, hatua ambayo inatishia makubaliano ya kibiashara baina ya Marekani, Mexico na Canada, biashara ambazo ni manufaa kwa Trump katika kuwania muhula wa pili wa Urais.

Ongezeko hilo la ushuru kwa bidhaa zinazotoka Mexico pia linatishia kuuharibu uhusianao baina ya mataifa hayo mawili ambayo uchumi wake unashikana.

Rais wa Mexico, Andres Manuel Lopez Obrador alimuandikia barua Rais Trump akimwambia matatizo ya kijamii hayasuluhishwi kupitia ushuru ama kwa njia za kutishiana huku akiongeza kwamba Marekani ina historia ya kuwa nchi ya wahamiaji. Rais Anders Manuel alimfahamisha Trump kwamba hahitaji kuzozana naye na anapendekeza kuongeza vikao vya mazungumzo kutafuta njia mbadala kwa tatizo la wahamiaji.

Mexiko: Präsident Lopez Obrador
Picha: picture-alliance/A. Nava

Waziri wa masuala ya Kigeni wa Mexico, Jesús Seade, amesema tangazo la Trump ni hatari sana.

"Tangazo hilo iwapo litatekelezwa litakuwa jambo zito sana na hatari, wakati huo huo sio siri kwamba Trump ni mraibu katika matumizi ya mtandao wa kijamii wa Twitter. Sisemu tutakaa tu kusubiri hadi Juni 10 kuona iwapo atatekeleza ama hatatekeleza alilolisema, ila naamini hiki ni kitu kisichofaa kutekelezwa kwa sababu kitakuwa kitu kibaya sana," alisema Seade.

Trump anaamini Mexico imeshindwa kuwazuilia wahamiaji

Rais Trump amekuwa akiilaumu Mexico kwa kushindwa kuzuilia ongezeko la wakimbizi kutoka nchi kama El Salvador na Honduras wanaopitia mpaka wa Mexico kuingia Marekani.

Uamuzi huu wa ghafla wa Trump kwa Mexico ulitolewa wakati Marekani yenyewe imekuwa ikisukuma kupitishwa kwa makubaliano ya kibiashara kwa Amerika ya Kaskazini na pia amefanya uamuzi huu chini ya wiki mbili baada ya kuondoa ushuru wa shaba na vyuma kutoka Mexico na Canada siku ambayo Trump na Rais wa Mexico pia walianzisha mazungumzo ya kuratibu makubaliano hayo ya kibiashara. Makubaliano hayo yanahitajika kuidhinishwa na wabunge kutoka nchi zote tatu za Marekani, Mexico na Canada.

Tayari soko la hisa la bara la Asia na Ulaya limeathirika na tangazo hilo la Trump na kusababisha kushuka kwa hisa za kampuni za magari za Japan.

(APE/AFPE)