1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza kuwania urais 2024

16 Novemba 2022

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwania tena wadhifa huo kwenye uchaguzi wa 2024 baada ya kushindwa mwaka 2020, ingawa msaidizi wake mkuu, bintiye Ivanka, amesema hatoungana na baba yake safari hii.

https://p.dw.com/p/4Jand
USA | Trump will bei Wahl 2024 erneut antreten
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

"Mabibi na mabwana, wageni waheshimiwa na raia wenzangu, Marekani inaanza sasa kurejea kwenye utukufu wake." Trump alishangiriwa na mamia ya wafuasi wake wakati akitangaza azma yake ya kuwania tena urais akiwa kwenye jumba lake la Mar-a-Lago jimboni Fllorida, wiki moja baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula, ambao chama chake cha Republican kilishindwa kupata viti vingi ilivyovitarajia kwenye baraza la Congress.

Kwenye hotuba yake iliyochukuwa takribani saa zima, Trump aliwaambia wafuasi hao waliojazana kwenye ukumbi uliopambwa kwa mataa na bendera za Marekani kwamba anadhamiria kuirejeshea nchi yake utukufu wake ambao alianza kuujenga kwenye utawala wake wa miaka minne, lakini akakatishwa njiani mwaka 2020 na utawala wa Joe Biden ambaye alidai ameiuwa kabisa ndoto ya Wamarekani.

"Lakini daima tumejuwa kwamba huo haukuwa mwisho. Ulikuwa ni mwanzo tu wa mapambano yetu kuikowa ndoto ya Marekani. Ili kuirejeshea Marekani utukufu na heshima yake, usiku huu natangaza kuwania urais wa Marekani." Alisema Trump.

Siasa za kimataifa

Indonesien Krisentreffen bei G20-Gipfel
Rais Joe Biden wa Marekani anatuhumiwa na Donald Trump kwa kuivunja 'Ndoto ya Wamarekani'.Picha: The Yomiuri Shimbun via AP Images/AP Photo/picture alliance

Kwenye hotuba hiyo, Trump alitumia muda mrefu kuyalinganisha mafanikio yake wakati akiwa rais na utawala wa sasa wa Biden. Na kama kawaida yake, alitumia kauli chafu dhidi ya wahamiaji, huku akiitaja miji yaMarekani kuwa imegeuka majalala yaliyojaa uhalifu na damu kutokana na wageni. 

Kuhusu siasa za kimataifa, Trump alisema utawala wake ulizidhibiti nchi hasimu kama vile Iran na Urusi. 

"China, Urusi, Iran na Korea Kaskazini zilidhibitiwa. Na kuheshimiwa. Waliiheshimu Marekani na kwa ukweli hasa, waliniheshimu mimi. Niliwajuwa vyema. Niliwajuwa vyema." Alisema mwanasiasa huyo.

Ivanka hataungana na baba yake

USA | Ivanka Trump
Ivanka TrumpPicha: CNP/MediaPunch/imago images

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, binti yakeIvanka, ambaye alimchaguwa kuwa mshauri mkuu na maalum kwenye utawala wake, amesema kwamba hataungana na baba yake kwenye mbio za kuwania tena urais. 

"Nampenda sana baba yangu. Mara hií nimechaguwa kuwaweka mbele watoto wangu wadogo na maisha ya faragha kama familia. Sipangi kuingia kwenye siasa. Ingawa nitampenda na kumuunga mkono baba yangu siku zote, nitafanya hivyo nje ya jukwaa la siasa. Ninashukuru kuwahi kuwatumikia Wamarekani na daima nitajifaharishia mafanikio mengi ya utawala wetu." Aliandika kupitia mtandao wa Twitter.

Kwa upande wake, Biden amekataa kusema lolote kuhusu tangazo la Trump kuwania tena urais, ingawa kwenye ukurasa wake wa Twitter ametuma video kuikosowa rikodi ya Trump alipokuwa madarakani.