Trump asema siku za karibuni zitakuwa muhimu kuelekea kupona
4 Oktoba 2020Vidio hiyo kutoka kwa rais Trump , ambaye anatibiwa katika hospitali ya jeshi, inakuja baada ya taarifa zinazokinzana kusababisha mkanganyiko kuhusiana na hali yake kiafya.
Trump alikuwa amevaa suti bila tai na alikuwa amekaa wakati akirekodi ujumbe wake huo. Alisikika kidogo akiwa anashindwa kuzungumza na akipumua kwa taabu.
"Nafikiri nitarejea hivi karibuni," alisema, na kuongeza kwamba anapambana kupona virusi hivyo kwa ajili yake binafsi na pia kwa dunia kwa ujumla.
"Ni lazima nirejee kwasababu bado tunapaswa kuifanya Marekani kuwa kubwa tena," alisema , akitumia kauli mbiu ya kampeni yake.
Amesema "anaanza kujisikia vizuri " lakini siku za hivi karibuni zitakuwa mtihani halisi wa kupona kwake, na amewashukuru waungaji mkono wake wa ndani ya nje ya nchi hiyo kwa kumtakia kupona haraka na "mapenzi yao makubwa."
Daktari wake Sean Conley aliwaambia waandishi habari mapema kuwa hali ya Trump inaendelea vizuri, na kusema timu ya madaktari "ina furaha kubwa kwa maendeleo anayopitia rais."
Hali yake ilikuwa inatia wasi wasi
Hata hivyo , chanzo kingine kimewaambia waandishi habari kwamba ishara muhimu za Trump zilikuwa zinatia wasi wasi.
"Ishara muhimu za rais katika muda wa masaa 24 zilikuwa zinatia wasi wasi mno na masaa 48 mengine yatakuwa muhimu kwa maana ya huduma anayopewa. Bado hatuko katika njia ya wazi kuelekea kupona kabisa ," chanzo hicho kimewaambia waandishi habari wa Ikulu ya Marekani ya White House wanaosafiri pamoja na rais.
Taarifa hiyo iliyotolewa na chanzo hicho ilikuwa inakanganya, wakati inakuja dakika chache baada ya madaktari kutoa taarifa kwa umma, na ilitolewa kwa masharti ya kutotajwa jina. Ikulu ya White House imekataa kusema lolote zaidi.
Kituo cha televisheni cha FOX wakati huo huo kimeripoti kuwa Trump alionesha "hali ambayo si nzuri" za kupona kutoka hali ya kawaida hadi mbaya kabla ya kupelekwa katika kituo cha afya cha Walter Reed, kituo cha afya cha jeshi nje ya mji wa Washington, siku ya Ijumaa.
Hata hivyo , ripoti hiyo imemnukuu afisa mwandamizi wa utawala huo akisema kwamba "katika muda wa masaa 12 yaliyopita hakukuwa na wasi wasi kabisa."
Kumekuwa pia na ukosefu wa uwazi juu ya muda wa maambukizi ya rais huyo pamoja na lini alipimwa.