Trump asaini maagizo kadhaa ya rais
21 Januari 2025Trump amewasamehe takriban watu 1,500 waliovamia majengo ya bunge mnamo Januari 6, 2021, katika ishara muhimu kwa watu waliowashambulia polisi walipokuwa wakijaribu kuwazuia wabunge kuthibitisha kushindwa kwake katika uchaguzi wa 2020.
Trump amesema, "Tunataka nchi yenye umoja. Walisema usizungumzie wafungwa wa Januari 6 ambao utawaachilia leo. Bwana, usiweke hilo kwenye hotuba yako tafadhali."
Soma pia: Rais Trump aanza awamu mpya kwa kishindo
Rais Trump pia ametia saini maagizo ya kutangaza uhamiaji haramu katika mpaka wa Marekani na Mexico kama dharura ya kitaifa, inayolenga wahalifu, mashirika ya kigaidi, pamoja na uraia kwa watoto waliozaliwa Marekani wa wahamiaji nchini humo kinyume cha sheria.
Agizo la Trump kuhusu suala la kuwapa wakimbizi makazi mapya Marekani litasimamishwa kwa angalau miezi minne akihoji kwamba Marekani haina uwezo wa kuhifadhi idadi kubwa ya wahamiaji.
Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyengine tena ameiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa mazingira wa Paris.
Kwa kufanya hivyo, Trump ameiondoa nchi ambayo ndiyo mtoaji mkubwa wa gesi chafuzi duniani kutoka kwenye juhudi za ulimwengu za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa mara ya pili katika kipindi cha mwongo mmoja.
Katika hotuba yake baada ya kula kiapo, Trump alisema kwamba Marekani itaanza tena uchimbaji wa mafuta na gesi baada ya hatua hiyo kusitishwa na rais aliyeondoka mamlakani Joe Biden.
Soma pia: Biden aonya juu ya tishio kwa demokrasia Marekani
Migogoro ya afya na uhuru wa kujieleza
Amri nyingine ya rais Trump iliiondoa Marekani kutoka kwa Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, kwa madai kwamba shirika hilo lilishughulikia vibaya janga la UVIKO pamoja na migogoro mengine ya afya kimataifa.
Hata hivyo rais huyo mpya wa Marekani, amesema anataka kuweka sifa ya kuwa mmoja wa viongozi watakaoleta amani na mshikamano.
Trump na washirika wake wa chama cha Republican wamekuwa wakituhumu utawala wa Rais wa zamani kwa kuhimiza ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza kwenye majukwaa ya mtandaoni.
Na mara moja alitia saini agizo kuu ambalo amesema linalenga kile alichokitaja kama "kurejesha uhuru wa kujieleza na kukomesha udhibiti wa shirikisho."
Huku haya yakijiri China imesema kuwa inatumai kushirikiana na Marekani, kutatua masuala ya biashara, baada Trump kutishia kutoza ushuru mkubwa kwa bidhaa za China.