Trump akutana na Xi Jinping, Florida
7 Aprili 2017Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa China Xi Jinping walianza mkutano wao katika hoteli ya mapumziko ya Rais Trump iliyopo jimbo la Florida, kwa kujadili kitisho cha mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini pamoja na mvutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Trump amesema yeye na Xi wameunda urafiki wakati wa zira hiyo, na wakati wa mkutano wao Trump alikubali kuizuru China, katika siku za karibuni. Trump alisema kuwa yeye, mke wake Melania Trump, Xi na mke wake Peng Liyuan walikutana kwa chakula cha jioni katika hoteli yake ya Mar-a-Lago lakini kabla ya hapo alikutana na Xi kwa majadiliano marefu aliyoyataja kuwa hayakuwa na mafanikio yoyote.
Kabla ya mkutano huo, Trump alilalamika juu ya mikataba mibaya ya kibiashara kati ya Marekani na China na kutaja kuwa hilo litakuwa miongoni mwa mada za mkutano wao.
"China haikuwa ikitutendea haki na tumekuwa tukikubali mikataba mibaya ya kibiashara kutoka China kwa miaka mingi. Hilo ni moja ya mambo tutakayo yajadili. Jambo lingine bila shaka itakuwa Korea Kaskazini. Na kwa namna fulani hayo mawili yatachanganyika. Hivyo tutazungumzia juu ya biashara, Korea Kaskazini, na mambo mengine mengi," amesema Donald Trump.
Msemaji mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying amesema kabla ya mazungumzo hayo kuwa kwa upande wa Xi, mkutano huo ni muhimu sana katika kuamua mwelekeo wa mahusiano ya China na Marekani katika enzi mpya, pamoja na kukuza amani, utulivu na mafanikio katika eneo la Asia ya Pasifiki na hata dunia nzima.
Hata hivyo, ziara ya Xi iligubikwa na mfululizo wa mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Marekani katika moja ya kambi ya jeshi la anga nchini Syria, kama jibu kwa shambulio la silaha za kemikali lililofanywa wiki hii dhidi ya raia wa Syria, ambalo Marekani inamlaumu Rais Bashar al-Assad .
China ni taifa lenye kura ya turufu na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na mara kadhaa imekuwa ikisema kuwa mgogoro wa Syria unahitaji suluhisho la kisiasa.
Lakini kwa mara sita imekuwa ikiiunga mkono Urusi kupitia kura yake ya turufu, kuzuia jitihada za baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa za kuuchukulia hatua mgogoro wa Syria.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape/dpae
Mhariri: Gakuba Daniel