1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aichimbia 'mkwara' Mexico

Caro Robi
27 Januari 2017

Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto amefutilia mbali ziara Marekani baada ya Donald Trump kutia saini agizo la rais la kutaka kuanza kujengwa kwa ukuta katika mpaka kati ya Marekani na Mexico na kuitaka Mexico kugharamia.

https://p.dw.com/p/2WU8Q
Bildkombo Enrique Pena Nieto Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP/G. Herbert/S. Walsh

Trump amependekeza bidhaa za Mexico zinazoingizwa Marekani zitozwe kodi ya asilimia 20 ili kugharamia ujenzi wa ukuta huo mpakani. Trump ameapa kuifanya Mexico kulipia gharama za ujenzi huo ambao unalenga kuwazuia wahamiaji haramu kuingia Marekani, suala ambalo Mexico imesisitiza haitafanya.

Msemaji wa Ikulu ya White House Sean Spicer amesema wazo la kutozwa kodi ya asilimia 20 bidhaa kutoka Mexico ni mojawapo tu ya mapendekezo ya kufikia azma ya kuujenga ukuta huo. Waziri wa mambo ya nje wa Mexico Luis Videgaray amesema nchi yake ina nia ya kufanya mazungumzo na Marekani ili kudumisha uhusiano mzuri lakini kugharamia ujenzi wa ukuta sio jambo la kujadiliwa.

Siku 7 madarakani Trump, kachukua hatua kubwa

Trump amewataka wabunge wa Republican kuchukua hatua za haraka kutekeleza ajenda kadhaa ikiwemo ujenzi huo, kupunguza kodi na kutangua sheria ya bima ya afya kwa wote maarufu Obamacare.

Kombi-Bild Donald Trump Theresa May
Rais Donald Trump na Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May

Akiwahutubia wabunge hao wa Republican katika jimbo la Philadelphia ambako wanakutana kwa mkutano wa kilele wa siku tatu, Trump amewaambia watu wa kawaida Marekani ndiyo watakaonufaika na sera zake.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amewahutubia wabunge wa Republican katika mkutano huo wa Philadelphia na kusema Marekani na Uingereza zina jukumu la kuushajaisha uhusiano wao alioutaja wa kipekee na kusema huenda wakaongoza tena chini ya enzi mpya.

May aliyasema hayo kabla ya mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana na Trump hii leo. Atakuwa  kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni kuizuru Marekani chini ya utawala mpya wa Trump. Uingereza inatafuta kufikia makubaliano kati yake na Marekani kufuatia uamuzi wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Steinmeier amuonya Trump kuhusu Iran

Wakati huo huo, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani anayeondoka kutoka wadhifa huo Frank Walter Steinmeier amesema Ujerumani ina tofautiana  na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu matumizi ya mateso na masuala mengine na kumuonya kiongozi huyo mpya wa Marekani dhidi ya kuyavunja makubaliano yaliyofikiwa na Iran kuhusu mpango wake wa kinyuklia akisema itakuwa kosa kubwa ambalo linaweza kuchochea vita Mashariki ya kati.

Steinmeier mit Verdienstorden der Ehrenlegion ausgezeichnet
Waziri wa mambo ya nje anayeondoka wa Ujerumani Frank Walter SteinmeierPicha: Picture-Alliance/dpa/S. Kunigkeit

Steinmeier anayetarajiwa kuwa rais mpya wa Ujerumani kuanzia mwezi ujao ameliambia gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung kuwa alishtushwa na uchaguzi wa Marekani uliofanyika mwaka jana na kwamba anatumai kuwa sasa Trump atabadilika baada ya kuingia rasmi madarakani.

Steinmeier amesema anatumai kuwa utawala mpya wa Marekani utaona umuhimu wa kuwepo ushirikiano kati yake na Ulaya kwani ndiyo msingi wa nchi za magharibi unaohitaji kudumishwa na kuongeza Marekani haitanufaika kutokana na Ulaya kudhoofika. Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kuzungumza na Trump kwa mara ya kwanza hapo kesho kupitia njia ya simu.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo