Toledo, Marekani. Maandamano ya Wanazi mamboleo yazusha ghasia.
16 Oktoba 2005Katika jimbo la Ohio nchini Marekani , watu kadha wamekamatwa baada ya maandamano yaliyopangwa kufanywa na kundi la Wanazi mamboleo kuzusha ghasia zilizowahusisha watu wanaopinga maandamano hayo.
Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na kuwakamata watu kadha baada ya watu hao kufanya ghasia na uharibifu katika mitaa wakiharibu magari na kutia moto duka moja la vinywaji vikali katika mji wa Toledo.
Meya wa mji huo Jack Ford ameelekeza lawama zake kutokana na ghasia hizo kwa kundi la wahalifu ambao wamechukua nafasi hiyo ya hali ya wasi wasi kuweza kufanya uhalifu wao.
Ghasia hizo ziliongezeka kwa mapambano kati ya raia wa Kizungu ambao hujihisi wao ni jamii bora zaidi ambao wanatoka katika kundi lenye makao yake makuu mjini Virginia la National Socialist Movement pamoja na makundi ya mji huo ambayo yanahusika katika matayarisho ya upinzani wa maandamano hayo.