TLS yakosoa visa dhidi ya Wamaasai walioko Ngorongoro
20 Agosti 2024Tamko la chama hicho lifuatia maandamano ya amani yaliyofanywa na wamasai hao wanapinga hatua za mamlaka nchini humo kusitisha huduma muhimu ikiwemo shule na hospitali.
Huku kikitoa kauli ya kupinga vikali hatua zote zinazochukuliwa na mamlaka juu ya wakazi hao wanaotajwa kuwa wa asili katika eno hilo, TLS pia imetangaza kuunda kamati ya wataalamu wa sheria kwa ajili ya kutathmini hali jumla ya mambo katika eneo hilo.
Soma pia: HRW: Tanzania yawafurusha maelfu ya Wamaasai
Rais wa chama hicho aliyeingia katika nafasi hiyo hivi karibuni, wakilli Boniface Mwabukusi amesema kamati hiyo imepewa muda siku 30 kuchunguza na kutathimini yale yote yanayoendelea katika eneo hilo na inaanza kutekeleza majukumu yake Agosti 21.
Serikali imekuwa ikiratibu hatua za kuwaondoa wakazi hao
Serikali imekuwa ikiratibu mchakato wa kuwaondoa wakazi hao, ambao inasisitiza kuwa umekuwa ukifanyika kwa hiari na kwenda kuwatafutia makazi mapya katika eneo jipya la Msomera lililopo mkoani Tanga.
Hata hivyo, hatua hiyo bado imekuwa ikiandamwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya makundi, na hivi karibuni kabisa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) lilisema kutowasikiliza Wamaasai wanaioshi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni kuwanyima haki zao.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa TEC Padri Charles Kitima alihoji hatua za mamlaka kueleza wale wanataka kubaki katika eneo hilo wanafanya hivyo kwa hiari yao huku wakinyimwa haki zao za msingi ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Ripoti kutoka eneo la Ngororongoro zinasema Wamasai wamekuwa wakikusanyika na kutoa matamko ya kulaani kunyimwa huduma muhimu wakisema pamoja na hatua hiyo wataendelea kusalia katika eneo.
Baada ya familia kadhaa kuamua kuanzisha makazi mapya huko Msomera, eneo hilo sasa limesaliwa na kata 11 yenye vijiji 25.
Sikiliza zaidi: