1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tillerson: Hatma ya Assad itaamuliwa na Wasyria

30 Machi 2017

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson amesema majadiliano zaidi yanahitajika kufanyika kuhusu Syria, lakini mustakabali wa Rais Bashar al-Assad utaamuliwa na watu wa Syria wenyewe.

https://p.dw.com/p/2aMWk
Mevlut Cavusoglu   Rex Tillerson Treffen in Ankara
Picha: picture alliance/AA/R.Aydogan

Akizungumza leo kwenye mji mkuu wa Uturuki, Ankara baada ya kukutana na viongozi wa Uturuki, Tillerson ameisifu Uturuki kama mshirika muhimu katika juhudi za kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na amesema 'hakuna pengo' kati ya Uturuki na Marekani katika dhamira yao ya kupambana na kundi hilo.

Kauli hiyo ameitoa wakati akijibu swali kuhusu Marekani kuliunga mkono kundi la wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria, YPG, kundi ambalo Uturuki ambayo ni mshirika wa Marekani katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO, inaliona kama adui.

Syrien Qamischli PG Einheit
Wapiganaji wa YPGPicha: Reuters/R. Said

Aidha, Tillerson amesema mazungumzo yao yalijikita katika malengo matatu, ikiwemo kufanya kazi kwa pamoja kupambana na IS, kujenga uwezo wa kuwepo utulivu katika ukanda huo pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Uturuki.

''Uturuki imekuwa mshirika wetu wa NATO tangu mwaka 1952 na tutaendeleza ushirikiano wa kijeshi ndani ya NATO na kwenye muungano wa kimataifa kupambana na IS. Mazungumzo yetu yamethibitisha kwamba tutazuia kuanza tena kwa mashambulizi ya IS kwenye maeneo waliyokuwa wanayashikilia awali na kuzuia kuibuka kwa vitisho vya kigaidi pamoja na magaidi kusajiliwa katika mtandao,'' alisema Tillerson.

Wasyria kuamua mustakabali wa Assad

Ama kwa upande mwingine Tillerson amesema mustakabali wa Rais Assad utaamuliwa na wananchi wa Syria. Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani amesema muda wa kubakia madarakani Assad uko ndani ya maamuzi ya Wasyria wenyewe.

Chini ya utawala wa Barack Obama, Marekani ulilifanya suala la kuondoka madarakani Rais Assad kama sera muhimu, lakini rais mpya wa nchi hiyo, Donald Trump anazingatia zaidi kuliangusha kundi la IS.

Türkei Besuch US-Außenminister Tillerson
Rex Tillerson (kushoto), Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildrim (katikati) na Mevlut CavusogluPicha: picture-alliance/dpa/Prime Minister's Press Service/Stf

Cavusoglu amesema Uturuki inatarajia ushirikiano mzuri na utawala wa Rais Trump katika suala la wanamgambo wa Kikurdi wa Syria na kuongeza kuwa hatua yoyote ya Marekani kuwaunga mkono wapiganaji wa YPG, utamaanisha kuwa mustakabali wa Syria uko katika hatari.

Wakati huo huo, Cavusoglu amekielezea kitendo cha kukamatwa mjini New York, kwa afisa mtendaji wa benki ya Uturuki ya Halkbank kuwa cha kisiasa. Afisa huyo anatuhumiwa kwa kuisaidia Iran kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo. Inadaiwa afisa huyo alikula njama na mfanyabiashara wa dhahabu mwenye uraia wa Uturuki na Iran, Reza Zarrab, ambaye tayari kesi yake inaendelea nchini Marekani.

Cavusoglu amesema mwanasheria aliyefungua kesi dhidi ya Zarrab ana uhusiano wa karibu na wafuasi wa kiongozi wa kidini anayeishi nchini Marekani, Fethullah Gulen, anayeshutumiwa kwa kupanga jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Uturuki mwaka uliopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AFP
Mhariri: Saumu Yusuf