Tetesi za uhamisho wa wachezaji barani Ulaya zapamba moto
16 Juni 2023Lo Celso kwenye rada ya Barcelona.
Barcelona wamemuweka kiungo wa kati wa Tottenham Giovani Lo Celso kwenye orodha ya wachezaji wanaolengwa katika majira ya kiangazi.
Bosi wa Barcelona Xavi anavutiwa sana na mchezaji huyo na amemweka miongoni mwa viungo vyake vya kutafuta sokoni.
Barca wako tayari kujadili dili la Lo Celso na Spurs iwapo watakubaliana huenda wakamrejesha Clement Lenglet ambaye alikuwa Spurs
Lenglet amerejea Barca kufuatia mkopo wa msimu mzima na anasalia kwenye orodha ya wachezaji wanaolengwa na Spurs.
Barca wanatazamia kusajili angalau kiungo mmoja mpya, huku pia nyota wa Manchester City Ilkay Gundogan akiwa kwenye rada ya kutimkia Barcelona, Gundogan atakuwa mchezaji huru Julai 1 .
Bernardo Silva na Manchester City bado kizungumkuti.
Man City haitaweka kiwingu kwa Bernardo Silva kama anataka kuondoka katika klabu hiyo.
Klabu ya Paris Saint-German ya nchini Ufaransa ina nia ya kumsajili mchezaji huyo huku pia Barecelona wakitajwa kuingia katika rada hizo za mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno.
Msimu uliomazika Manchester City wamekuwa na wakati mzuri na timu hiyo bado inayo nia ya kutaka kumbakisha nyota huyo kwa muda mrefu, akiwa na timu yake msimu huu wameshinda Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Premia na Kombe la FA.
Hata hivyo, Silva anatajwa kuwa anafikiria kuondoka City msimu uliopita wa joto, jambo ambalo halikutimia.
Dili la Declan Rice lawakosesha amani washika mitutu wa London.
Klabu ya soka ya Arsenal imegonga mwamba kwa wagonga nyundo wa London West Ham baada ya ofa yao ya awali ya pauni milioni 80 kukataliwa, Nahodha wa West Ham na nyota wa kimataifa wa England, Declan Rice anawindwa na klabu za Arsenal, Manchester City, Bayern Munich na Manchester United.