Tetemeko la Ardhi laua watu zaidi ya 2000 Afghanistan
10 Oktoba 2023Utawala wa Afghanistan umesema matetemeko kadhaa yameikumba magharibi mwa nchi hiyo mwishoni mwa wiki na leo Jumatatu, na kusema baadhi yalisikika hadi katika nchi jirani ya Iran.
Kwa mujibu wa mamlaka, watu zaidi ya 2000 wamekufa na wengine wapatao 9,240 wamejeruhiwa. Shirika la Jiolojia la Marekani limesema matetemeko hayo yamefikia kipimo cha 6.3 kwenye kipimo cha Richter katika mji wa Herat magharibi mwa Afghanistan.
Tetemeko hilo liliharibu angalau vijiji 13 katika wilaya ya Zindah Jan mkoani Herat na katika majimbo kadhaa, watu wanaendelea kukusanya misaada kwa ajili ya waathiriwa.
Maafisa wa uokoaji wanaendelea kuwatafuta watu walionusurika pamoja na miili ya wahanga wa tetemeko hilo huku Uturuki, Iran na Pakistan zikiahidi kutoa huduma za dharura na misaada ya kibinadamu.
Wafanyakazi wa kujitolea wakiwa kwenye malori yaliyosheheni chakula, mahema na mablanketi wameendelea kuwasili katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa yanayopatikana takriban kilomita 30 kaskazini-magharibi mwa mji wa Herat.
Wakazi na wauguzi katika eneo hilo la Herat wameliambia shirika la habari la dpa kuwa matetemeko hayo yalikuwa makubwa mno na watu walijificha katika maeneo ya wazi kama bustani na viwanja vya michezo.
Soma pia: Tetemeko lingine la kipimo cha 4.9 laikumba Afghanistan
Atiqullah, mkazi wa eneo Zanda Jan huko Herat anaeleza:
"Tetemeko lilipotokea asubuhi ya leo, tuliondoka nyumbani kwetu na kukimbilia kwa jamaa zetu. Hali ni tete mno. Natumai serikali na mashirika ya kimataifa yataweza kuwasaidia wakaazi walioathiriwa na maafa haya haraka iwezekanavyo."
Matatizo ya afya ya akili kutokana na matetemeko hayo
Kulingana na Daktari mmoja, tetemeko la ardhi la siku ya Jumamosi limeathiri vibaya afya ya akili ya watu, na kusema wagonjwa wengi wanasumbuliwa na tatizo la mshtuko na wasiwasi.
Msemaji wa wizara ya usimamizi wa majanga Mullah Janan Sayeq amewambia wanahabari katika mji mkuu Kabul kuwa ripoti kutoka maeneo ya tukio, zinaelezea "hali mbaya sana", huku watu wakiendelea kuwatafuta na kujaribu kuokoa familia zao kutoka kwenye vifusi.
Soma pia: Watu zaidi 2,000 wafa kwa tetemeko la ardhi Afghanistan
Hata hivyo, kuna ripoti zinazokinzana kuhusu idadi kamili ya vifo na majeruhi. Serikali imetangaza vifo 2,053 na zaidi ya watu 1,200 waliojeruhiwa, huku Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ikisema imejumuisha vifo 1,023 na watu 1,663 waliojeruhiwa. OCHA imeongeza kuwa zaidi ya watu 11,000 wameathiriwa na mkasa huo.
Wakati majira ya baridi yakikaribia, suala la kutoa makazi kwa watu waliokumbwa na matetemeko hayo ya ardhi litakuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Taliban nchini Afghanistan, ambayo ilichukua madaraka mnamo Agosti mwaka 2021 na ambayo ina uhusiano mbaya na mashirika ya misaada ya kimataifa.