Tanzania yasherehekea sikukuu ya Eid al-Adha leo
21 Julai 2021Ni katika sala ya Eid kitaifa mjini Dar es saalam iliyohudhuriwa na mamia ya waumuini wa dini ya kiislamu wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali na kidini .
Katika sala hii iliyofuatiwa na baraza la Eid ujumbe wa kila kiongozi wa kidini na kiserikali ni kuhakikisha waumini wanajifunza namna ya kuishi na janga la corona ambalo hadi sasa limeendelea kuathiri watu mbalimbali nchini humo, kwani kwa mujibu wa serikali watu zaidi ya mia nne wanapokea matibabu kutokana na kuathiirika na virusi vya Corona huku zaidi ya mia mbili wakipokea matibabu makubwa ikiwemo usaidizi wa hewa ya oksijeni.
Waziri mkuu nchini humo Kassimu Majaliwa amesema, serikali kwa kutambua kwamba taifa hilo sio kisiwa na watu wake wanahitaji kushirikiana na watu wengine duniani ikiwemo biashara na kijamii hivyo hakuna budi kuhakikisha wanaweka huduma za chanjo ili huduma hiyo muhimu kwa dunia ya sasa ipatikane nchini.
Katika baraza hilo ambalo hutumiwa mara zote na viongozi wa waumini wa kiislam katika kupenyeza ujumbe wao kwa mamlaka na waumini wamesema, Kila muumini katika taifa anawiwa kujifunza kuishi na janga hilo, kadhalika kufuata taratibu za miongozo ya imani hiyo katika kukabiliana na maradhi ya mlipuko kama ilivyoelekezwa katika dini.
Ustaadhi Nour Jabir Mruma katibu mkuu wa (BAKWATA) amesisitiza kwamba, kuna haja serikali kuendelea kutoa elimu ya chanjo ya Corona kwani mengi yanayoendelea katika mitandao ya kijamii yanaleta hofu kwa wale wenye nia ya kutaka kuchanjwa kwakuwa tayari serikali imeweka ni hiyari.
Kukamilika kwa baraza hilo kumetoa nafasi kwa waumini wenye uwezo kutekeleza ibada ya kuchinja kwa ajili ya Mola wao na kisha sehemu ya kitoweo kugawa kwa masikini na mafakiri. Huu ni muongozo katika imani hiyo.
Sherehe visiwani Zanzibar
Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi leo, kwa mara ya kwanza tangu kuingia madarakani mwaka jana, ameongoza waumini wa dini ya kiislam katika sala na baraza la eid iliyofanyika kisiwani pemba wakati ambapo kumeibuka malalamiko ya chama cha ACT-wazalendo,kilichomo ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar, juu ya matokeo ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Konde.
Sherehe hizo za kitaifa zimefanyika Wete kisiwani Pemba wakati ambapo chama cha ACT wazalendo kinajadili ni hatua zipi watazichukuwa katika kuonesha kutoridhika na matokeo yaliyokipa ushindi chama cha CCM na baadhi ya wananchi wa Wete walisusia sala hiyo.
Licha ya kuendeleza wito kwa wananchi kudumisha umoja na Amani nchini, rais hakugusia chochote kuhusu uchaguzi huo unaolalamikiwa ambapo baadhi ya wafuasi wa chama cha ACT-wazalendo wanakhofu na kuendelea kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Kabla ya kumkaribisha Rais Mwinyi waziri wa ofisi ya Rais Katiba na Sheria Haroub Ali Suleiman aliwapongeza wananchi wa Pemba kwa kuhudhuria kwa wingi.
Katika sala na baraza la Idi iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, na makamu wa kwanza anayetoka chama cha ACT-wazalendo na makamu wa pili Hemed suleiman Abdulla na rais mstaaafu Dk Amani Karume, Rais Mwinyi pia alisisitiza wananchi kuendeleza mapambano dhidi ya udhalislishaji wa watoto na kijinsia, pamoja na madawa ya kulevya, sambamba na kila mtu kuhubiri Amani na kuchukuwa tahadhari juu ya korona.
Habari hii imeandikwa na Hawa Bihoga na Salma Said