1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaripoti kifo chake cha kwanza kutokana na corona

31 Machi 2020

Tanzania imethibitisha kifo cha kwanza kutokana na maradhi ya COVID-19 yanayosababishwa na virusi vya corona. Mhanga huyo ni Mtanzania hambaye amefariki dunia leo alfajiri katika hospitali ya Mlongazila .

https://p.dw.com/p/3aFAE
Taiwan Taipei | Übung gegen Ausbreitung des Coronavirus
Picha: picture-alliance/AP Images/Yomiuri Shimbun

Taarifa za kifo cha Mtanzania huyo zilizotolewa na waziri wa afya Ummy Mwalimu zinaonekana kuwashtua wengi na zinakuja huku  maambukizi ya virusi hivyo yakizidi kuongezeka.

Katika taarifa yake, Waziri Ummy amesema Mtanzania huyo aliyetambulishwa kwa jina la Idd Mbita alikuwa na umri wa miaka 49, na anakuwa mtu wa kwanza kupoteza maisha kutokana na virusi hivyo tangu vilipopiga hodi kwa mara ya kwanza nchini Machi 16.

Taarifa hiyo inasema " Nasikitika kutangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa COVID-19 hapa nchini kilichotokea alfajiri ya leo katika kituo cha matibabu ya wagonjwa wa COVID-19 kilichopo Mlongazila, Dar es salaam. Marehemu pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine,” mwisho wa kunukuu.

Kifo hicho kinakuja wakati takwimu za wizara ya afya zikionyesha kwamba hadi sasa watu walioambukizwa virusi hivyo wakifikia 19, huku mmoja akiwa amepona.

Kwa ujumla ingawa vyombo vya habari vinaendelea kutoa nafasi kubwa ya kuwaasa wananchi kuchukua tahadhari juu ya janga hilo, hata hivyo bado maisha ya wananchi wengi ni yale yale ya siku zote, wakiendelea kutangamana na kushiriki shughuli zao za kila siku.

Bunge ambalo limeanza vikao vyake leo Jumanne,  limelazimika kubadili muundo wake, ambako kwa wakati huu kunashuhudiwa idadi ndogo ya wabunge wakiruhusiwa kuingia ukumbini na muda wa kuendesha vikao hivyo, ukipunguzwa kutoka saa 11 kama ilivyokuwa imezoeleka hadi kufikia saa nne kwa siku.

Vikao hivyo huanza saa nane mchana na kumalizika jioni ya saa 11 tofauti na zamani ilipokuwa ikianza saa tatu asubuhi na kudumu hadi jioni. Baadhi ya wabunge wameanza kuonyesha wasiwasi wao kutokana na janga hilo, na mmoja wao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye anataka umakini zaidi wa serikali katika kukishughulikia kitisho hicho.

Kumekuwa na juhudi za usafishaji wa mazingira kama vile kuanza upuliziaji wa dawa ya kuua vimelea vya vijijidu kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam ikiwemo maeneo yanayokusanya idadi kubwa ya watu kama kituo cha mabasi cha ubungo.