1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yapokea Faru weusi tisa kutoka Afrika Kusini

George Njogopa 11 Septemba 2019

Serikali ya Tanzania imepokea faru weusi tisa kutoka nchini Afrika Kusini, kama hatua ya kukabiliana na upungufu wa wanyama hao ambao katika miaka ya hivi karibuni walitoweka kwa wingi kutokana na matukio ya ujangili.

https://p.dw.com/p/3PPlB
Namibia Nachhaltiger Tourismus
Picha: DW/C. Springate

Ujio wa faru hawa ni matokeo ya jitihada za pamoja, baina Serikali ya Tanzania na wadau katika Uhifadhi ikiwemo shirika la Grumeti, ambalo limeratibu na kufadhili shughuli hii ili kufanikisha lengo la kuongeza idadi ya Faru angalau kwa asilimia 5 kwa mwaka.

Ndege iliyowabeba faru hao iliwasili katika uwanja wa ndege kimataifa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania na baada ya hapa wamesafirishwa hadi katika eneo maalum la kuwahifadhi, katika pori tengefu la Ikorongo ambalo linapakana na Hifadhi ya taifa ya Serengeti.

Kulingana na mkurugenzi wa wanyamapori, Dr Maurusi Msuha, wanyama hao ambao ni mchanganyiko wa faru dume na jike watapelekwa katika hifadhi mbalimbali nchini Tanzania.Idadi ya ndovu na faru yaongezeka tena Tanzania

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupokea idadi kubwa ya faru kutoka nje ya nchi, na kulingana na naibu waziri wa maliasili na utalii, Constantine Kanyasu faru hao watalindwa kwa gharama yoyote, kuhakikisha hawapungui kama ilivyotokea kwenye miaka ya 1970-1980.

Südafrika Schwarzes Rhinozeros ohne Horn
Faru mweusi Picha: picture-alliance/dpa/J. Hrusa

Ukichochewa na biashara haramu ya bidhaa za wanyama kama pembe na ngozi, ujangili umeathiri kwa kiwango kikubwa hali ya uhifadhi nchini Tanzania, huku mojawapo ya wanyama walioathirika zaidi wakiwa ni faru ambapo katika kipindi cha miaka 40 Tanzania imepoteza asilimia 99 ya faru wake.

Hata hivyo, katibu mkuu wa wizara ya maliasi na utalii Profesa Adolf Mkenda, amesema Tanzania imejifunza kutoka yale yaliyopita na hali hiyo haitarajii ikaachwa iendelee kutokea tena.

Kifaru mweupe apata mimba

Kulingana na takwimu za shirika la uhifadhi duniani la IUCN katika miaka ya 70 Tanzania ilikadiriwa kuwa na faru 10, 000 huku Serengeti pekee ikiwa na wanyama hao wapatao 700. Hata hivyo, idadi ya faru hao imepungua hadi kufikia113.

Shirika hilo limetangaza wanyama aina ya faru weusi ambao wapo 750 katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF), Tanzania imepoteza takribani asilimia 98 ya faru weusi. Hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala alizindua mpango wa taifa wa miaka mitano (2019 - 2023) wa usimamizi na uhifadhi wa faru weusi Tanzania.

George Njogopa