1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yabadili mpango mapambano dhidi ya Ukimwi

Florence Majani24 Novemba 2023

Wizara ya Afya nchini Tanzania leo imezindua mpango mpya wa kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya ngono na homa ya ini kwa pamoja, huku tafiti zikionyesha ongezeko la magonjwa ya ngono nchini humo.

https://p.dw.com/p/4ZPhz
Mapambano dhidi ya Ukimwi | Waziri wa afya Tanzania Ummy Mwalimu
Waziri wa afya Tanzania Ummy MwalimuPicha: Prosper Kwigize/DW

Akizindua mpango mkakati mpya wa kudhibiti kwa pamoja magonjwa ya Ukimwi, Magonjwa ya ngono na homa ya ini, Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu, amesema takribani watu 6,542 walibainika kuwa na magonjwa ya ngono katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu.

Waziri Ummy amesema idadi hiyo inaakisi kuwa bado kuna juhudi zaidi zinahitajika katika kukabiliana na magonjwa ya kujamiiana.

Magonjwa makubwa ya ngono ni Kaswende, Kisonono na mengine yanayoathiri via vya uzazi.

Akasema  magonjwa ya ngonoyana uhusiano mkubwa na maambukizi ya VVU na homa ya ini hivyo serikali imeona ni vyema kuja na mkakati wa kuyadhibiti kwa pamoja

Soma pia:Mabadiliko ya tabianchi yanatishia vita dhidi ya Ukimwi

utafiti uliofanywa katika kipindi cha 2016-17-umeonyesha kuwa ugonjwa wa kaswende ulikuwapo mara tano zaidi kwa watu wenye VVU na kwa watu wasio na VVU ni 0.8.

"Kwa takwimu hizi ni muhimu kuwa na mpango jumuishi kama taifa katika kukabiliana na maradhi haya." Alisema Waziri Ummy.

Mpango mpya wa kukabiliana na Ukimwi

Waziri Ummy amesema,kuanzia sasa mpango wa taifa wa kudhibiti ukimwi, umebadilishwa na kuwa mpango wa taifa wa ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini (NASHCOP).

Wadau wa afya katika mkutano huo, walielezwa kuwa, hali ya maambukizi ya VVU kwa vijana wa miaka 15 hadi 24bado ni kubwa huku maambukizi hayo yakiendelea kushika kasi zaidi kwa madereva wa masafa marefu, wavuvi na wanaofanya kazi za migodini.

"Bado tunakabiliwa na changamoto ya maambukizi kwa vijana wetu,." Alisema waziri wa afya Tanzania.

Wakati takwimu hizo zikionyesha hali mbaya kwa vijana, Pudensiana Mbwiliza,  Mwenyekiti Wa Jukwaa La Vijana Wanaoishi Na Virusi Vya Ukimwi Tanzania amesema unyanyapaa ndicho chanzo cha vijana wengi kushindwa kupima magonjwa ya ngono na Ukimwi.

Soma pia:Lengo la kutokomeza Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria hatarini

Dr Neema Mlole ambae ni Mratibu wa huduma za UKIMWI Idara ya Afya , Ustawi wa jamii na Lishe  amesema Mpango uliozinduliwa ni kwa ajili ya kuunganisha huduma za afya, ambazo awali mifumo ilikuwa inajikita katika kupima Ukimwi pekee lakini sasa, mifumo hiyo itaangalia pia upimaji wa magonjwa mengine ya ngono na homa ya ini.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) Christine Musanhu,  amesema huduma jumuishi si rahisi  kama inavyoonekana na huenda likawa jambo gumu,

Uzinduzi wa mpango huu umekuja katika kipindi ambacho dunia inatarajia kuadhimisha siku ya ukimwi duniani, mnamo Desemba 1 mwaka huu ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajia kuzindua pia takwimu mpya za hali ya VVU nchini.