1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Mahakama yamtia Zitto Kabwe hatiani

George Njogopa29 Mei 2020

Mahakama ya kisutu nchini Tanzania imemtia hatiani kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kwa makosa ya uchochezi, lakini imemwachia huru kwa sharti la kutotoa au kutoandika uchochezi katika kipindi cha mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/3cxSd
Tansania Dar es Salaam | Zitto Kabwe, Partei Zitto Kabwe
Picha: DW/E. Boniphace

Mwanasiasa huyo ametiwa hatiani leo katika mashtaka ya uchochezi kutokana na matamshi yake aliyoyatoa miaka miwili iliyopita. Zitto aliyetinga mahakamani hapo akiwa ameonyoa kipara anadaiwa kuyatenda makosa ya uchochezi Oktoba 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Hukumu hiyo hata hivyo, imezua mjadala mkubwa na chama chake kinasema kinaendelea kuitafakari. Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Dorothy Semu amesema bado ni mapema mno kusema kwamba wataikatia rufaa.

Hukumu hiyo imekuwa ikitazamwa kwa namna mbalimbali na kikubwa zaidi kinachojitokeza ni suala la uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Je, uamuzi huo utamuathiri vipi kisiasa?

Wengi wanaanza kudadisi nafasi ya mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kigoma mjini namna atakavyoweza kusimama katika majukwaa ya kisiasa kunadi sera zake na za chama chake bila kutoa shutuma ilihali tayari anakabiliwa na sharti la kimahakama.

Ama, Zitto amekuwa na ufuasi mkubwa katika mitandao ya kijamii kutokana na namna anavyoibua mijadala na kukosoa baadhi ya mambo yanayoendelea serikalini.

Wachambuzi wanahoji huenda uamuzi huo ukamuathiri kisiasa
Wachambuzi wanahoji huenda uamuzi huo ukamuathiri kisiasaPicha: DW/S. Khamis

Kuhusu shauri lake hilo, Februari 18 mwaka huu Zitto alikutwa na kesi ya kujibu na hivyo kuanza kujitetea kwa siku nne mfululizo kutoka Machi 17 hadi 20.

Madai ya mauaji ya polisi dhidi ya raia

Mashtaka ya Zitto yanatokana na kauli zake za kulitaka jeshi la polisi kutolea maelezo kile alichokiita mauaji ya polisi dhidi ya raia yaliyotokea kwenye Kijiji cha Mpeta, Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma. Utetezi wake ulianza ikiwani ni siku chache baada ya kurejea nchini baada ya kumaliza ziara yake katika mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani na Uingereza.

Ziara hiyo ilizua gumzo nchini Tanzania hususani baada ya Zitto kubainisha wazi kuiandikia barua Benki ya Dunia kusitisha mkopo wa elimu kwa Tanzania.

Baadhi ya wanansiasa wa chama tawala CCM walidaiwa kutoa kauli za kutishia uhai wa mwanasiasa huyo huku yeye mwenyewe akidai kuwa kumekuwa na mipango ya "kumbambikia kesi ya uhujumu uchumi."