1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania kuwasilisha ripoti ya haki za binaadamu

Admin.WagnerD25 Februari 2020

Serikali ya Tanzania itawasilishi ripoti yake kuelezea hali jumla ya haki za binadamu nchini humo katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu unaoendelea Geneva, Uswisi. 

https://p.dw.com/p/3YPCv
Aussenminister Palamagamba Kabudi von Tansania
Picha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Ikiwa katika maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi mkuu ambao kwa kawaida hufanyika mwezi Oktoba, Tanzania imepanga kuwasilisha ripoti yake ikifafanua kwa kina kuhusu mazingira jumla ya haki za binadamu.

Ripoti hiyo itakayowasilishwa na waziri wamashauri ya kigeni Profesa Palamagamba Kabudi anayehudhuria mkutano huo, itagusia masuala yanayohusu ulinzi wa haki za binadamu, uboreshwaji wa huduma za kijamii na masuala mengine yahusuyo elimu.

Waziri Kabudi amesema Tanzania itatumia fursa hiyo kutoa mwelekeo halisi namna uchaguzi wa mwaka huu utakavyofanyika na kwamba ripoti hiyo itakuwa imemulika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Tansania Sansibar Pemab Polizisten in Mannschaftswagen
Picha hii inayonyesha polisi wakiwa wanapiga doria katika mitaa ya Visiwani Zanzibar Machi, 2016Picha: picture-alliance/dpa

Ingawa kumekuwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wachunguzi wa masuala ya haki za binadamu wanaoituhumu Tanzania kuziendea kinyume haki hizo, serikali imekuwa ikizikanusha tuhuma hizo, kwa hoja kwamba wale wanaoinyoshea kidole hawajui mukhtadha kamili kuhusu nafasi ya Tanzania katika kulinda haki za binadamu.

Hata hivyo, wakosoaji wa mambo wanasema kiwango cha kubinywa uhuru wa maoni, kubanwa kwa wanasiasa kufanya shughuli zao na kudhibitiwa kwa vyombo vya habari ni baadhi ya mambo yanayoshuhudiwa kwa wingi wakati huu.

Na wakati huu kuelekea katika uchaguzi mkuu, kilio cha wanasiasa wa upinzani ni kile cha miaka yote kudai tume huru ya uchaguzi. Wanasiasa hao wamekuwa wakipendekeza kufanyika kwa marekebisho madogo ya katiba yatayowezesha kuundwa kwa tume nyingine kabla ya uchaguzi wenyewe.

Hoja hiyo imekuwa ikipingwa vikali na serikali kwa maelezo kuwa imekosa mashiko na hapo jana, Katibu Mkuu wa chama tawala, Bashiri Ally aliwakosoa wale wanapigania katiba hiyo akisema huu siyo muda muafaka kuzungumzia suala hilo.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam