1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZambia

Tanzania kuiuzia Zambia mahindi ya dola milioni 250

30 Juni 2024

Tanzania itaiuzia Zambia tani 650,000 za mahindi katika mpango unaonuiwa kusaidia taifa hilo la kusini mwa Afrika kupunguza uhaba wa chakula unaosababishwa na ukame wa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/4hh3q
Zambia |
Kundi la watu wakizungumza baada ya kupokea chakula kilichotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).Picha: Guillem Sartorio/AFP/Getty Images

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema nchi hizo mbili zimetia saini makubaliano ya kusambaza nafaka hiyo, inayotarajiwa kulisha takriban watu milioni 7.

Soma pia: Zambia yaagizia maelfu ya tani za mahindi kutoka Tanzania

Bashe ameongeza kuwa makubaliano hayo na Zambia, yatatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi minane huku Tanzania ikipata dola milioni 250 katika biashara hiyo.

Mkataba huo ulisainiwa na Andrew Komba, mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi ya Chakula ya Tanzania inayomilikiwa na Serikali (NFRA), na mratibu wa maafa wa Zambia, Gabriel Poleni.

Zambia inakabiliwa na ukame ambao umepunguza uzalishaji wa umeme na chakula, na hivyo kupelekea serikali kuagiza chakula kutoka nchi jirani.