Tanzania: Magufuli au Demokrasia?
27 Oktoba 2020Matendo ya awali ya John Pombe Magufuli akiwa Rais wa Tanzania, yalishangiliwa nyumbani na nje ya nchi akitajwa kuwa mpiganaji mkubwa dhidi ya rushwa na mfano wa kuigwa barani Afrika.
Alihakikisha hospitali zinakuwa na vitanda vingi zaidi badala ya sherehe kubwa za kitaifa, akafanya ziara za kukagua wizara na mamlaka, akapunguza kabisa safari za nje ya nchi kwa mawaziri.
Licha ya kuwa mwanachama wa chama tawala kilicho madarakani kwa muda mrefu CCM, Magufuli aliibua upya matumaini ya mabadiliko ya demokrasia mnamo mwaka 2015. Hata hivyo muda mfupi kabla ya uchaguzi wa Rais na wabunge, mambo ni tofauti.
Hakuna tena uhuru wa vyombo vya habari
“Rais Magufuli hajafanikisha kitu chochote kizuri,” anadai Mkuu wa taasisi ya Konrad Adenauer jijini Dar es salaam Daniel El-Noshokaty. Anasema Magufuli alijaribu kuwapa wananchi matumaini, miradi kadhaa ya miundombinu kama vile mradi wa reli uliotekelezwa na ada kwa shule za sekondari zilifutwa. Lakini bado nchi imebeba mzigo mkubwa wa madeni na ahadi kuu ya Magufuli katika uchaguzi ya kupambana na rushwa haijafanikiwa.
Soma zaidi:Guterres atoa wito wa uchaguzi huru na wa haki Tanzania
Badala yake, Magufuli anaonekana kupambana na wapinzani wake wa kisiasa kwa kuchukua hatua kali. Katika mahojiano yake na DW, El-Noshokaty, anasema hakuna tena uhuru wa habari Tanzania kwani wapinzani hukamatwa na kufanyiwa dhulma.
Ananukuu ripoti ya shirika la waandishi wasio na mipaka inayosema "Tanzania imeporomoka kwa nafasi 53 katika faharisi ya uhuru wa habari, na kwamba hakuna nchi duniani iliyowahi kuporomoka kwa kiwango hicho. El-Noshokaty anaongeza kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi, simu binafsi za wagombea wa upinzani zilizuiliwa na mtu hakuweza hata kutuma ujumbe wa simu.
Lissu mwenye matumaini
Moja ya wagombea waliyozuiliwa ni Tundu Lissu. Mwanasiasa wa chama cha upinzani cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA. Mwanasiasa huyu wa upinzani ndiye hasimu mkubwa wa Magufuli katika uchaguzi ujao. Lissu mwanasheria mwenye miaka 52, alikuwa uhamishoni Ubelgiji alipokuwa akiishi kwa miaka mitatu. Aliponea chupuchupu kuuawa baada ya jaribio la kutaka kumuua kushindikana Septemba 2017 ambapo alipigwa risasi 16. Waliofanya jaribio hilo la mauaji hadi sasa hawajulikani na polisi walishasimamisha uchunguzi.
Katika kampeni zake za uchaguzi, Lissu ameonyesha shauku kubwa. Mikutano yake ya kisiasa imehudhuriwa na watu wengi na chama muhimu zaidi kwa upande wa Zanzibar ACT Wazalendo, kinamuunga mkono Lissu. Hili limebadilisha hali hasa kwa vijana, anasema Mkuu wa taasisi ya Konrad Adenauer jijini Dar es salaam Daniel El-Noshokaty. “Vijana wengi unawasikia sasa wanazungumzia suala la siasa na wanataka kupiga kura. Kabla ya hapo walikuwa hawajali tena siasa zinazoendelea hapa nchini."
Soma zaidi:Tanzania yajiandaa kwa uchaguzi Oktoba 28, 2020
Lissu mwenyewe kujiamini: "Maandalizi yetu ya uchaguzi wa Oktoba 28 ni mazuri sana," alisema mwanasiasa huyo wa upinzani katika mahojiano na DW siku chache kabla ya uchaguzi. "Tumetuma waangalizi wetu kwa kila kituo cha kupigia kura nchini kote. Kwa kweli tunakabiliwa na vizuizi kadhaa vya hapa na pale kutoka serikalini, lakini hadi sasa tuna hakika kuwa tutashinda kwa asilimia 60 hadi 70."
Lakini hata msemaji wa Chama tawala, Humphrey Polepole, naye anajiamini. Katika mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopita alisema "Tulifanya kampeni ya uchaguzi iliyoboreshwa kisayansi, asilimia 89 ya mikutano yetu ilifanyika mapema asubuhi. Watu wengi walifanikiwa kumsikiliza mgombea wetu wa Urais John Magufuli kuliko tulivyotarajia." Hivyo anatarajia ushindi wa kishindo kwa rais huyo anayetetea kiti chake.