1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taliban wazidi kufagia miji Afghanistan, dunia yashtushwa

13 Agosti 2021

Kundi la Taliban limeteka miji mikubwa zaidi Ijumaa huku likielekea kwenye udhibiti kamili wa Afghanistan na kuzidi kuusogelea mji mkuu Kabul, mnamo wakati Marekani na Uingereza zikituma wanajeshi kuondoa raia wao Kabul.

https://p.dw.com/p/3yxzj
Afghanistan Update Bildergalerie Taliban Kämpfer Kandahar
Wapiganaji wa Taliban wakiwa juu ya gari la polisi lililoharibiwa kandoni mwa barabara mjini Kandahar, Agosti 13, 2021.Picha: AFP via Getty Images

Katika muda wa masaa 24, mji wa pili na wa tatu kwa ukubwa nchini Afghanistan - Herat ulioko magharibi na Kandahar ulioko kusini, imeangukia mikononi mwa waasi wa Taliban kama ilivyotokea kwa mji mkuu wa mkoa wa Helmand, ambako vikosi vya Marekani, Uingereza na Jumuiya ya kujihami NATO, vilipigana moja ya mapambano makali zaidi katika mzozo huo.

Soma pia: Taliban yaombwa kujiunga na serikali

Wapiganaji wa Taliban pia wameuteka mji mkuu wa mkoa wa Logar - Pul-e-Alam, ulioko umbali wa kilomita 50 tu kutoka Kabul. Mapema leo, maafisa na wakaazi mjini Kandahar, walisema vikosi vya serikali vilijiondoa kwa wingi na kukimbilia kambi ya kijeshi nje ya mji huo wa kusini mwa Afghanistan. Saa kadhaa baadae, Taliban wakasema wamechukua pia udhibiti wa Lashkar Gah, ambao ni mji mkuu wa mkoa jirani wa Helmand.

Pul-e-Khumri, Afghanistan | Taliban
Bendera ya Taliban inaonekana kwenye mnara huku watu wakikusanyika katika uwanja mkuu wa mji wa Pul-e-Khumri, Agosti 11, 2021, baada ya Taliban kuuteka mji huo mkuu wa mkoa wa Baghlan.Picha: AFP/Getty Images

Kimsingi serikali sasa imepoteza sehemu kubwa ya nchi kufuatia kampeni kali ya kijeshi ya Taliban iliyodumu kwa siku nane tu na ambayo imeishtua hata Marekani, ambayo ni mfadhili mkuu wa serikali mjini Kabul.

Soma pia: Kundi la Taliban lauteka mji wa 10 Afghanistan

Umoja wa Mataifa sasa unatahadharisha juu ya mzozo mkubwa wa kibinadamu unaoinyemelea nchi hiyo. "Mzozo huu umeongezeka kwa kasi kubwa sana kuliko tulivyotarajia, na hali ina viashiria vya janga la kibinadamu," amesema Thomson Phiri, msemaji wa shirika la chakula la umoja huo WFP.

Wimbi la kwanza la mashambulizi lilianzishwa mapema mwezi Mei baada ya Marekani na washirika wake kuondoa vikosi vyao kutoka Afghanistan, huku rais Joe Biden akisistiza dhamira yake ya kumaliza miongo mwili ya vita kufikia Septemba Mosi.

Nguvu yaelekezwa mijini

Mzozo huo umeongezeka pakubwa tangu mwezi Mei, wakati vikosi vinavyoongozwa na Marekani vilipoanza hatua ya mwisho ya kuondoa wanajeshi wake. Baada ya miezi kadhaa ya kuchukuwa kile kilichodhaniwa kuwa maeneo ya vijijini yasio ya kimkakati, Talibani wakaelekeza nguvu na mawazo yao kwenye miji.

Kandahar, Afghanistan | Kämpfe zwischen Taliban und Afghanischer Armee
Moshi ukitanda baada ya mapigano kati ya Taliban na jeshi la serikali ya Afghanistan mjini Kandahar, kusini-magharibi mwa Kabul, Agosti 12, 2021.Picha: Sidiqullah Khan/AP Photo/picture alliance

Waasi hao wamechukua zaidi ya dazen moja ya miji mikuu ya mikoa katika wiki moja iliyopita na kuuzingira mji mkubwa zaidi eneo la kaskazini, katika ngome ya asili ya upinzani dhidi ya Taliban wa Mazar-i-Sharif, ambao hivi sasa ni moja ya michache inayoendelea kutoa upinzani.

Soma zaidi:Afghanistan: Mikoa zaidi yaingia mikononi mwa Taliban

Uingereza hii leo imekosoa hatua ya Marekani kuondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan, na kusema kuwa kurudi kwa Taliban kutatengeneza mazingira kwa makundi ya itikadi kali yanayoitishia dunia.

Chanzo: Mashirika