1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taliban wamkamata mpiganaji aliemuuwa mwanamke wa Hazara

19 Januari 2022

Mpiganaji wa Taliban amekamatwa kwa kumpiga risasi na kumuua mwanamke wa Kihazara kwenye kituo cha ukaguzi katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul, wakati akirejea nyumbani kutoka harusini. Mauaji yamewatia hofu wanawake.

https://p.dw.com/p/45ly0
Ghasni Afghanistan
Picha: Hector Retamal/AFP

Mauaji ya mwanamke huyo, Zainab Abdullah mwenye umri wa miaka 25, yaitokea katika kiunga cha mji wa Kabul kinachokaliwa hasa na wanachama wa jamii ya wachache ya Washia wa kabila la Hazara, ambao wamekandamizwa na Wasunni wenye msimamo mkali kwa karne kadhaa, ambapo makundi ya itikadi kali kama vile Dola la Kiislamu huwalenga mara kwa mara katika mashambulizi mabaya.

Abdullah aliuawa "kimamosa", Msemaji wa Taliban Mohammed Naeem alisema kwenye mtandao wa Twitter, na kuongeza kwamba mpiganaji aliyekamatwa ataadhibiwa.

Soma pia: Kabul: Zaidi ya watu 30 wauawa kwenye mlipuko wa bomu

Familia yake imepatiwa kiasi cha Afhani 600,000 (takribani dola 5,700) kama fidia ya mauaji hayo yaliyotokea Januari 13 katika kiunga cha mji mkuu cha Dasht-e-Barchi, ilisema wizara ya mambo ya ndani katika maelezo tofauti.

Afghanistan Kabul Proteste von Frauen gegen Beschränkungen durch Taliban
Wanawake wa Afghanistan wakiandamana kupinga kupunguza haki zao baada ya Taliban kutwaa madaraka.Picha: ALI KHARA/REUTERS

Baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake wamepanga maandamano madogo madogo mjini Kabul tangu mauaji ya Abdullah, wakitaka haki itendeke.

Wanawake waelezwa kutiwa hofu

"Tuliposikia kuhusu mauaji ya Zainab tuliingiwa na hofu. Tunaogopa kwamba iwapo tutatoka majumbani mwetu tunaweza tusirudi wazima," alisema mwanaharakati wa haki za wanawake aliyeomba kutotajwa jina lake kwa sababu za kiusalama.

"Majira ya usiku hatuwezi kutoka nje na hata wakati wa siku za mchana hatutoki nje isipokuwa tu kama kuna jambo la dharura," alisema, na kuongeza kwamba kupitia vituo vya ukaguzi lilikuwa jambo la hatari kwa wanawake.

Soma pia: Watu 27 wauawa wakimkumbuka kiongozi wa Kishia Kabul

Mapema mwezi huu, polisi ya kidini ya Taliban ilichapisha mabango katika mji mkuu ikiwaamuru wanawake kujifunika. Msemaji wa wizara inayohofiwa ya masuala ya ukuzaji wa maadili na kuzuwia maovu, alisema lilikuwa ni himizo tu kwa wanawake wa Kiislamu kufuata shariah.

Deutschland, Frankfurt | Protest für die Evakuierung gefährdeter Afghanen
Watu wakiandamana mjini Frankfurt, Ujerumani, kupinga utawala wa Taliban.Picha: Daniel Kubirski/picture alliance

Siku ya Jumanne, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, alilihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa "kuwawajibisha" wale wenye hatia ya ukiukaji nchini Afghanistan.

Alisema kuwanyima wanawake na wasichana haki zao za msingi ni jambo linaloharibu sana kwa taifa ambalo tayari linakabiliwa na janga la kibinadamu lisilo kifani.

Soma pia: UN: Watoto wengi wameuwawa Afghanistan 2016

Taliban wameahidi kuwa na mtazamo laini wa sheria zilizoainisha utawala wao wa kwanza kuanzia 1996 hadi 2001, lakini serikali yao ya muda haina wajumbe wanawake.

Chanzo: AFPE