1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Ta'azia: Askofu Mkuu Desmond Tutu, mwanaharakati asiyechoka

26 Desemba 2021

Akiwa mmoja kati ya wapambanaji wakubwa wa ubaguzi wa rangi katika karne ya 20 nchini Afrika Kusini, Desmond Tutu alisalia kuwa mkosoaji wa siasa za nchi hiyo na za kimataifa maishani mwake mote.

https://p.dw.com/p/44qHE
Anglikanische Geistliche und Menschenrechtler Desmond Tutu verstorben
Picha: Maurice Mcdonald/dpa/picture alliance

Askofu Desmond Tutu, aliyefariki dunia siku ya Jumapili (Disemba 26) akiwa na umri wa miaka 90, ni mmoja kati ya washindi muhimu kabisa wa Tuzo za Nobel kutoka Afrika Kusini na mpinzani asiyechoka wa mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Mnamo Aprili 1993, nchi yake ilikuwa kwenye kilele cha mabadiliko. Miaka mitatu kabla ya hapo, na baada ya miongo kadhaa ya ukandamizaji dhidi ya raia weusi, Rais Frederik Willem de Klerk alikuwa ametengaza mageuzi. Wafungwa wengi wa kisiasa, akiwemo Nelson Mandela, waliachiliwa na vyama ama mashirika yao hayakuwa tena marufuku. Lakini mazungumzo juu ya demokrasia mpya yalikuwa yamekwama.

Kisha, kundi moja la makaburu linalofuata siasa kali za mrengo wa kulia likamuuwa mwanasiasa mashuhuri na mpigania uhuru, Chris Hani, na kuifanya nchi kukaribia kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kwenye maziko ya Hani, ambayo yalihudhuriwa na watu 100,000, Desmond Tutu akaituliza hali kwa kuuongoza umati wa watu huku wakipiga mayowe: "Tutakuwa huru! Sote - weusi na weupe pamoja!"

Ilikuwa ni kwenye nyakati ngumu kama hizi katika historia ya Afrika Kusini ambapo Desmond Tutu alionesha nguvu zake. Maishani mwake mote, alifuata maadili yake bila ya kuyumba na kupigania Taifa la Ukole - dhana aliyoitunga mwenyewe kumaanisha taifa la Afrika Kusini - akitumia njia za amani na zisizo machafuko.

Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kupambana dhidi ya ukaburu

Südafrika Desmond Tutu und Egil Aarvik
Wakati wa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1984.Picha: Helmuth Lohmann/AP Photo/picture alliance

Akiwa amezaliwa kwenye mji wa migodi wa Klerksdorp mwaka 1931, kazi yake ya kwanza ilikuwa ni uwalimu, lakini akaiacha baada ya serikali kuanza utekelezaji wa sera zilizohujumu maendeleo ya kielimu ya wanafunzi weusi.

Tutu akachaguwa kazi mpya kanisani, akawa askofu wa kwanza mweusi wa Kanisa la Anglikana jijini Johannesburg na, baadaye, Askofu Mkuu wa Cape Town.

Hata alipokuwa kanisani na kwenye nafasi zote hizo kubwa, hakuwahi kusita kupambana dhidi ya ubaguzi wa rangi. Waziwazi alijitokeza kuunga mkono malengo ya chama cha Nelson Mandela, African National Congress (ANC), ambacho kilitaka kujenga Afrika Kusini ya kidemokrasia isiyogawika kwa makabila na rangi. Mwaka 1984, Tutu alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na juhudi zake zisizotumia nguvu dhidi ya utawala wa kikaburu.

'Siku ya aina yake'

Lakini tukio jengine mbali kabisa lilithibitisha kuwa muhimu zaidi kwake: Siku moja ya mwezi Aprili 1994, alipopiga kura yake kwenye uchaguzi wa kwanza huru na wa kidemokrasia wa Afrika Kusini.

Südafrika Desmond Tutu und Nelson Mandela
Akiwa na rafiki yake, Marehemu Nelson Mandela, baada ya uchaguzi wa 1994.Picha: David Brauchli/AP Photo/picture alliance

"Ni siku ya kipekee kwa watu wetu wote," alisema Tutu akionekana na furaha ya wazi akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha kupigia kura. "Na ninamaanisha watu wetu wote - weusi na weupe. Kwa sababu kwa sasa, hatutaweza kusema kwamba 'huu ni utawala haramu.' Itakuwa serikali yetu."

Haiba yake ya ucheshi na moyo msafi - ambayo aliendelea kuishikilia muda wote hata kwenye miaka ya fadhaa za mapambano ya haki - ilimtukuza kwa Waafrika Kusini walio wengi. Awali alikuwa amepanga kustaafu baada ya uchaguzi huo na kuishi nchini Marekani akiwa na wajukuu zake, lakini baada ya Rais Nelson Mandela kumuomba kuongoza Tume ya Ukweli na Maridhiano, iliyopewa jukumu la kuchunguza uhalifu wa wakati wa utawala wa kikaburu, aliamua kubakia nchini Afrika Kusini.

Maombi ya maridhiano

Tutu na tume hiyo walijaribu kusaka njia ya katikati baina ya haki ya washindi na msamaha, wakiomba yawepo maridhiano na msamaha. Kwa zaidi ya miaka mitatu, maelfu ya wahanga walipewa nafasi ya kuelezea masaibu yao, huku waliotenda uhalifu wakiomba msamaha.

Südafrika Desmond Tutu und der Dalai Lama
Akiwa na rafiki yake, Dalai Lama, mwaka 2015.Picha: Sanjay Baid/dpa/picture alliance

Akiwa kwenye joho lake la zambarau, mara kadhaa Tutu alijikaza asimwage machozi hadharani, lakini mara zote alielekeza macho kando yake, akisema mkazo unapaswa uwe kwa wahanga hao.

Kazi ya tume ilipokamilika, Tutu akendelea kuzungumzia dhidi ya dhuluma duniani kote: kutoka vita vya Iraq hadi tawala za kikandamizaji. Hakuwaacha hata majirani wa Afrika Kusini. "Ni askofu mdogo mwenye hasira na uchungu mwingi," ndivyo mtawala wa muda mrefu wa Zimbabwe, Robert Mugabe, alivyomuelezea baada ya Askofu Mkuu Tutu kutoa kauli ya kuukosowa utawala wake.

Tutu hakuwa mtu aliyesalia kupendeza miongoni mwa wengi kwenye chama tawala cha ANC pia - hasa pale alipopingana vikali na uhusiano wa serikali na Mugabe, kusita kwake kwenye vita dhidi ya UKIMWI na tabia ya wanasiasa kujilipa fedha nyingi.

Akiwa amevunjwa moyo na siasa za Afrika Kusini, baadaye alisema haikuwa tena jambo la lazima kuipigia kura ANC. "Watu wanauliza maswali, ambalo ni jambo jema. Hiyo ndiyo demokrasia."

Maisha ya faragha

Mwaka 1997, Desmond Tutu aligundulika kuwa na saratani ya kifuko cha mkojo. Miaka mitatu baadaye, kwenye sherehe za kutimiza miaka 79 tangu kuzaliwa, alitangaza rasmi kujiondowa kwenye shughuli zote za hadharani. Kwa njia yake ile ile ya utani, alisema anahitaji muda zaidi wa kunywa chai na mkewe.

Südafrika Desmond Tutu und seine Frau Leah Nomalizo Tutu
Akiwa na mke wake, Leah Nomalizo Tutu, mwaka 1999.Picha: Gail Oskin/AP Photo/picture alliance

Lakini hakufanya na asingeliweza kusalia kando kabisa kabisa ya siasa. Mwaka 2014, aliitisha mgomo dhidi ya kampuni za madini na mafuta. Mabadiliko ya tabianchi, alisema, yanatakiwa yapiganiwe kwa njia ile ile ambayo ubaguzi ulipiganwa katika miaka 1980. Akiwa muungaji mkono mkubwa wa haki za wapenzi wa jinsia moja, alisema yuko tayari kwenda motoni kuliko kumuabudu mungu mwenye chuki dhidi ya watu hao.

Binti yake, Mpho Tutu van Furth alimuoa mwanamke mwenzake nchini Uholanzi mwezi Disemba 2015. Akiwa mchungaji kwenye Kanisa Anglikana la Afrika Kusini, alipigwa marufuku kuendelea na kazi zake kwenye kanisa hilo. Akiwa mwenye afya iliyozorota, Askofu Tutu alihudhuria sherehe ya harusi ya pili ya binti yake huyo nchini Afrika Kusini mwezi Mei 2016, pale ndoa za jinsia moja zilipohalalishwa katika taifa hilo.

Matibabu ya saratani yalimfanya Desmond Tutu kuwa rahisi kupata maambukizo ya mara kwa mara. Katika miaka ya karibuni, Afrika Kusini ilikuwa ina wasiwasi sana na "Mkuu" wake - kama ambavyo Tutu alikuwa akiitwa kwa utani. Lakini mwanaharakati huyo wa haki za kiraia aliendelea kujitokeza hadharani kila alipopata nafuu.

Mwaka 2020, wakati wa maandamano ya 'Black Lives Matter' nchini Marekani, Tutu alisema ulikuwa "ukwlei mchungu" kwamba maisha ya makundi fulani katika jamii bado yanaonekana kuwa na thamani zaidi kuliko ya wengine.

Kauli hiyo ya hadhari kutoka kwa Tutu ilitokana na mauaji ya kusikitisha ya Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, George Floyd, akiwa mikononi mwa polisi.