1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yatishia kuidungua ndege yoyote ya Uturuki

Sylvia Mwehozi
19 Januari 2018

Syria imesema kwamba itaidungua ndege yoyote ya Uturuki itakayofanya mashambulizi nchini Syria, onyo linalokuja mnamo ambapo mvutano unazidi kuongezeka juu ya maandalizi ya jeshi la Uturuki kuvamia eneo la Wakurdi. 

https://p.dw.com/p/2r8YA
Kriegsflugzeug der türkischen Luftwaffe
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Gurel

Kutoka mjini Damascus naibu waziri wa mambo ya nje wa Syria Faysal Mekdad, alisema uingiliaji wa kijeshi katika eneo la Syria linalodhibitiwa na Wakurdi la Afrin litahesabiwa kuwa "tendo la kikatili". "Tunaonya kuwa jeshi letu la anga limerejesha uwezo wake wote na nguvu na liko tayari kuangamiza  ndege yoyote ya Kituruki katika anga ya Jamhuri ya Kiarabu ya Syria. Hii inamaanisha kuwa ikiwa kuna uchokozi wa aina yoyote wa ndege za Kituruki ndani ya Syria, haipaswi kuiona ni kazi rahisi," alisema Mekdad.

Mvutano huo unakuja baada ya Marekani kuainisha mipango yake ya kuunda kikosi madhubuti cha walinzi wa mpakani chenye wanajeshi 30,000 nchini Syria kinachoongozwa na vikosi vya jeshi la Syria lilitawaliwa zaidi na Wakurdi, baada ya kulishinda kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Uturuki ilijibu kwa hasira juu ya tangazo hilo.

Syrien YPG Kämpfer in Qamishli
Wafuasi na wapiganaji wa kundi la Kikurdi la Syria YPG wakipeperusha bendera mtaaniPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Uturuki inalichukulia kundi la wanamgambo wa Kikurdi la Syria linalodhibiti Afrin na maeneo mengine kando ya mipaka yake kama upanuzi wa wanamgambo ndani ya mipaka yake na inataka kuzuia uanzishwaji wa ukanda wa Kikurdi katika mipaka yake.

Marekani imeunda mahusiano ya karibu na wanamgambo wa Kikurdi kutokana na kuwa na maslahi sawa kwenye mapambano dhidi ya kundi la IS na pia imeweka ngome zake kaskazini mashariki mwa Syria .

Rais wa Uturuki Recep Tayyib Erdogan alikiita kikosi hicho kinachopendekezwa na Marekani kuwa "ni jeshi la kigaidi" na kuapa kuliangamiza. Alisema kwamba Uturuki itaanzisha mashambulizi makali dhidi ya eneo la Afrin na maeneo mengine ya Syria yanayodhibitiwa wanamgambo wa Kikurdi na ilikuwa ikipeleka idadi kubwa ya wanajeshi na mizinga kwenye mpaka wake.

YPG - Kurdische Miliz
Mpiganaji wa kundi la YPG la Syria Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Katika eneo la Afrin kwenyewe, wakazi waliandamana kupinga kitisho hicho cha Uturuki, kwa mujibu wa picha zilizochapishwa na shirika la habari la Kikurdi la Hawar. Walikuwa wakipeperusha bendera za wanamgambo wa kikurdi la YPG na pia mabango ya Abdullah Ocalan, kiongozi aliyeko jela wa chama cha wafanyakazi cha Wakurdi PKK ambacho Uturuki inakihesabu kama kundi la kigaidi.

Wanamgambo wa Kikurdi, ambao wanaongoza vikosi vya jeshi la Kidemkorasia la Syria, kwa hivi sasa wanadhibiti karibu asilimia 25 ya maeneo ya Syria na lilikuwa ni mshirika mkuu katika muungano wa jeshi unaongozwa na Marekani kwenye vita dhidi ya kundi la IS nchini humo.

Wakati huo huo, mkuu wa utumishi wa jeshi wa Uturuki na wakuu wa idara za usalama wamesafiri kuelekea Urusi kwa mazungumzo yanayotarajiwa kugusia uwezekano wa mashambulizi makali katika eneo la Afrin ambako jeshi la Urusi linaaminika kuwepo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi /AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman