1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yaomba mkutano wa jumuiya ya nchi za Kiarabu

14 Novemba 2011

Syria imeomba kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa jumuiya ya nchi za kiarabu, katika juhudi za kuzuia kutengwa na jumuiya hiyo.

https://p.dw.com/p/13ACU
Rais wa Syria anaekabiliwa na maandamano, Bashar al-Assad wa Syria
Rais wa Syria anayekabiliwa na maandamano, Bashar al-Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Syria imeomba kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa jumuiya ya nchi za kiarabu, katika juhudi za kuzuia kutengwa na jumuiya hiyo. Jumuiya ya nchi za kiarabu ilichukua uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Syria baada ya nchi hiyo kushindwa kusitisha vitendo vya umwagaji damu dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali ya Rais Bashar al Assad.

Mamia ya wasyria wanaounga mkono serikali walishambulia ofisi za ubalozi wa Ufaransa, Uturuki na Saudi Arabia kupinga uamuzi huo. Tangazo lililosomwa kwenye kituo cha televisheni ya Taifa limetaja kuwa sababu ya kuitishwa kwa mkutano huo ni kujadilili machafuko yanayoendelea na athari zake kwa mataifa ya kiarabu. Jumuiya ya nchi za kiarabu haijatoa jibu lolote kuhusu pendekezo hilo la Syria, na msimamo wa nchi 22 wanachama bado haujulikani bayana.

Proteste gegen Präsident Bashar Assad in Syrien
Waandamanaji wanaompinga rais Assad wakichoma picha yakePicha: picture-alliance/dpa

Uamuzi wa wiki iliyopita wa jumuiya ya kiarabu kuisimamisha uanachama Syria ulilenga pia kuiwekea vikwazo nchi hiyo kwa kushindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na jumuiya hiyo, katika juhudi za kuutanzua mgogoro wa kisiasa unaoikumba Syria kwa zaidi ya miezi minane.

Watu wengi wameuwawa

Umoja wa mataifa unakadiria kuwa watu 3,500 wengi wao wakiwa raia wamepoteza maisha katika kipindi hicho. Kufuatia uamuzi huo, maelfu ya watu wanaoiunga mkono serikali walifanya maandamano mjini Damascus, na kuzishambulia ofisi za ubalozi wa Uturuki, Saudi Arabia na Ufaransa.

Mmoja wa waandamanaji, Yousef Ahmad, alisema wanaamini kwamba uamuzi wa kuisimamisha nchi yao uanachama katika jumuiya ya nchi za Kiarabu ulishawishiwa na nchi za magharibi.

''Uamuzi uliochukuliwa dhidi ya Syria haulingani kabisa na utaratibu wa ushirikiano kati ya nchi za kiarabu. Sasa imekuwa dhahiri kuwa uongozi wa jumuiya hii unashawishiwa na msimamo wa Marekani na nchi nyingine za magharibi''. Alisema.

Baadaye polisi waliyatawanya maandamano hayo, lakini nchi ambazo balozi zao zilivamiwa zilivishutumu vikosi vya Usalama vya Syria kuzembea katika zoezi la kuzilinda ofisi zao. Wakati huo huo, Jumuiya ya nchi za kiarabu imetangaza kuwa itakutana na wawakilishi wa upinzani ambao unataka Rais Bashir Assad aondoke madarakani.

Mkutano wa wapinzani

Katibu mkuu wa jumuiya hiyo Nabil Elaraby alisema mkutano na wapinzani hao utafanyika Jumanne, lakini akaongeza kuwa bado ni mapema sana kuzungumzia suala la kuutambua upinzani huo kama mwakilishi halali wa nchi ya Syria. Tangazo la jumuiya ya nchi za kirabu kuisimamisha uanachama Syria halikujumuisha wito wa uingiliaji kijeshi katika nchi hiyo.

Uamuzi kama huo dhidi ya Libya ambao ulihimiza kuwekwa kwa eneo lisiloruhusiwa kuruka ndege, ulisaidia kushawishi baraza la usalama la umoja wa mataifa kupitisha operesheni za kijeshi za jumuiya ya kujihami ya NATO, chini ya kauli mbiu ya kuwalinda raia. Nchi nyingi za magharibi zilifurahia uamuzi wa jumuiya ya nchi za kiarabu kuisimamisha uanachama Syria, lakini Urusi imepinga uamuzi huo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AP

Mhariri: Josephat Charo