1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria, Urusi zakanusha kufanya shambulizi la sumu

6 Aprili 2017

Syria na Urusi zimekanusha tuhuma kuwa serikali ya Syria ndio iliyofanya shambulizi kali la silaha za sumu. Shinikizo linazidi kuwekewa jamii ya kimataifa kuchukua hatua

https://p.dw.com/p/2aoaI
Syrien Idlib Giftgasangriff
Picha: picture-alliance/ZUMA Wire/Syria Civil Defence

Ufaransa imesema imedhamiria kutafuta azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuchunguza vifo vya raia vilivyotokea katika mji wa kaskazini mashariki mwa Syria wa Khan Sheikhun, ambavyo Uturuki ilidai vilitokana na shambulizi la sumu la serikali ya Syria

Takribani watu 86 waliuawa mapema Jumanne katika shambulizi hilo huku wengine kadhaa wakipewa matibabu kutokana na matatizo ya kupumua na kutoa povu mdomoni. Mataifa yenye nguvu duniani yameinyooshea kidole serikali ya Bashar al-Assad, lakini Waziri wake wa Mambo ya Nje Walid Muallem amesisitiza kutohusika kwa serikali. "Nasisitiza tena kuwa jeshi letu halijawahi na halitawahi kutumia silaha za aina hiyo dhidi ya watu wetu na watoto na hata haliwezi kuzitumia dhidi ya magaidi wanaowaua watu wetu na watoto na wanaoshambulia usalama wa raia wetu kutumia makombora yao ya kiholela

Waziri wa Mambo ya kigeni Walid Muallem
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Syria Walid MuallemPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema azimio, lililowasilishwa na Uingereza, Ufaransa na Marekani linabakia kuwa suala la kipaumbele. Mshirika wa muda mrefu wa Syria, Urusi- imeyataja matukio hayo ya Khan Sheikhun kuwa ni "uhalifu mkubwa” lakini ikasema hakuna "habari za uhakika na zilizothibitishwa”.

Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema tuhuma zisizo na msingi kuhusu shambulizi hilo hazikubaliki kamwe kabla ya kufanyika uchunguzi.

Baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Usalama jana, wajumbe wa nchi za Magharibi wanatarajiwa kushinikiza kupigwa kura ikiwezekana leo kuhusu azimio linaloitisha uchunguzi kuhusu shambulizi hilo linalodaiwa kuwa sumu.

Russland Präsident Putin in Sankt Petersburg
Rais wa Urusi Vladmir Putin anasema Urusi haijahusikaPicha: picture-alliance/dpa/M. Metzel

Kama litadhibitishwa, litakuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya matumizi ya silaha za sumu katika vita vya wenywe kwa wenyewe nchini Syria, ambavyo vimewaua zaidi ya watu 320,000 tangu vilipoanza Machi 2011. Trump ameonya kuwa shambulizi hilo aliloliita la kinyama limeubadilisha mtazamo wake kuhusu Assad. "watoto wadogo, ambao ni wazuri sana. vifo vyao ni ukiukaji wa ubinaadamu. vitendo hivi vya kinyama vya utawala wa Assad haviwezi kuvumiliwa. Marekani inasimama na washirika wetu kote duniani kulaani shambulizi hili la kutisha na pia mashambulizi mengine ya kutisha". 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema ameridhika kuwa Marekani imeubadilisha mtazamo wake kumhusu Rais wa Syria Bashar al-Assad kufuatia shambulizi la sumu dhidi ya raia.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Muallem amesema kuwa uchunguzi wa aina hiyo "lazima uhakikishe kuwa hauingizwi siasa, na kwamba una uwakilishi mpana wa kijiografia na kwamba unaanzishiwa Damascus na sio Uturuki”.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba, Daniel