Syria: Wito wa kuungwa mkono watolewa
30 Agosti 2020Mwenyekiti mwenza wa upande wa upinzani kwenye Kamati ya Katiba ya Syria, Hadi al-Bahra, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva baada ya kumalizika mazungumzo ya wiki moja yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kwamba ana matumaini ya kufikia muafaka. Kamati hiyo ya wajumbe 45 inawajumuisha wawakilishi wa serikali, upinzani na asasi za kiraia, ina jukumu la kutayarisha katiba mpya itakayowezesha kufanyika kwa uchaguzi utakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Kamati hiyo ya Katiba iliundwa mnamo mwezi Septemba mwaka 2019 ilikutana kwa mara kwanza mwezi mmoja baada ya kuundwa kwake, lakini kutokana na kutokukubaliana juu ya ajenda zilizopangwa kujadiliwa pamoja na mkurupuko wa janga la virusi vya corona mikutano zaidi haikuweza kuendelea kufanyika hadi wiki iliyopita.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukijitahidi kwa zaidi ya miaka tisa kufikiwa azimio la kisiasa kuhusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchini Syria, ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 380,000 ambapo pia zaidi ya watu milioni 11wamelazimika kuyahama makazi yao.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo hayo, Geir Pedersen amesema japo kulikuwepo na baadhi ya mambo ambayo pande zinazohusika hazikufikia makubaliano lakini ameonesha matumaini kwamba imaendeleo mazuri yanaweza kupatikana kwa kuzingatia hatua ya kusitisha vita katika ngome ya mwisho ya waasi ya Idlib kaskazini magharibi mwa Syria iliyosimamiwa na Uturuki na Urusi mnamo mwezi Machi mwaka huu wa 2020.
Pedersen amesema mpaka sasa makubaliano hayo bado yanafanya kazi japo licha ya ukiukaji waq amkubaliano hayo wakati mwingine. Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa pia amefahamisha kuwa duru hii ya sasa ya mazungumzo imemalizika pasipo makubaliano yoyote katika ajenda muhimu au tarehe ya duru nyingine ya mazungumzo.
Mwenyekiti mwenza wa upande wa upinzani kwenye Kamati ya Katiba ya Syria, Hadi al-Bahra amesema makubaliano na upande wa serikari yalikuwa makubwa kuliko tofauti zilizojitokeza kati ya pande hizo.
Chanzo kutoka kwenye ujumbe wa serikali ya Syria kwenye mazungumzo hayo kimeliambia shirika la habari la serikali SANA, kwamba upande wa serikali una nia thabiti ya kuendelea kushiriki katika duru zijazo za mazungumzo.
Vyanzo:/ RTRE/AFP