Syria na Uturuki: Hali bado ni ya mvutano mjini Idlib
13 Februari 2020Shirika la habari la kitaifa nchini Uturuki Anadolu limemnukuu waziri huyo wa ulinzi Hulusi Akar akisema wamewapeleka wanajeshi wengine wa ziada katika eneo hilo ili kuhakikisha makubaliano ya kusitisha mapigano yanaheshimiwa.
Akar aliyazungumza hayo pembezoni mwa mkutano wa Jumuiya ya kujihami NATO mjini Brussels, huku akisema nguvu itatumika kwa wale wote watakaokiuka makubaliano ya usitishwaji wa mapigano hata kwa makundi ya itikadi kali. Akar ameishutumu Syria kwa kuimarisha mashambulizi yake katika eneo hilo.
Tamko la Akar limekuja baada ya Urusi kuishutumu Uturuki kushindwa kudhibiti makundi yalio na itikadi kali mjini Idlib kama ilivyokubalika katika makubaliano ya mwaka 2018. Idlib mji wa mwisho unaokaliwa na upinzani nchini Syria, unashikiliwa na makundi kadhaa ya wanamgambo likiwemo kundi la Hayat Tahrir al-Sham linaloongozwa na wanachama wa kundi la zamani lililokuwa na mafungamano na kundi la al Qaeda.
Vikosi vya rais Bashar al Assad vimeendelea na mashambulizi yake tangu mwezi Desemba na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 380, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la uangalizi la haki za binaadamu nchini humo.
Aidha mauaji ya wanajeshi 14 mjini Idlib kufuatia mashambulizi hayo ya serikali yamesababisha mvutano kati ya Ankara na Damascus huku Uturuki nayo mshirika wa karibu wa rais Assad ikionekana kuingia katika mvutano huo.
Hapo jana rais Erdogan aliishitumu Urusi kwa kutekeleza mauaji ya halaiki na kutishia kuvishambulia vikosi vyake popote vilipo nchini Syria iwapo wanajeshi wake wataumizwa tena au kuuwawa. Urusi nayo kupitia msemaji wake Dmitry Peskov imeishutumu Uturuki kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya mwaka 2018 ikisema Uturuki imejichukulia hatua yenyewe dhidi ya wanamgambo walio na itikadi kali mjini Idlib.
Huku hayo yakiarifiwa bunge la Syria leo limetambua mauaji ya mwaka 1915-1917 ya takriban warmenia milioni 1.5 kama mauaji ya Halaiki.
Bunge hilo limekosoa na kutambua mauaji hayo ya halaiki yaliofanyikwa wakati wa utawala wa Ottoman. Hata hivyo Uturuki inakataa shutuma za mauaji ya halaiki na kusema warmenia na waturuki waliangamia kufuatia vita vya kwanza vikuu vya dunia.
Huku hayo yakiarifiwa Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 700,000 wameachwa bila makaazi Kaskazini Mgharibi mwa Syria tangu mwezi Desemba kufuatia mashambulizi yanayoendelea yanayofanywa na serikali yanayolenga eneo la mwisho linalokaliwa na waasi.