1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria na Ukraine kutawala mkutano wa OSCE

8 Desemba 2016

Wakati Ujerumani inakamilisha muhula wa mwaka mmoja kama mwenyekiti wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE, Waziri wake wa Mambo ya Nje, Frank-Walter Steinmeier, ameitaka Urusi kushirikiana kikamilifu.

https://p.dw.com/p/2TwDE
Hamburg OSZE-Treffen  Steinmeier  Rede
Picha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Wito huo ameutoa jana usiku kabla ya kuanza kwa mkutano wa siku mbili wa OSCE mjini Hamburg, Ujerumani, ambao unatarajiwa kutawaliwa na ajenda kuhusu Syria na Ukraine. Wakati wa mkutano wake na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, siku moja kabla ya mkutano huo unaoanza leo, Steinmeier amesema Urusi inahitaji kusaidia kupunguza mivutano inayoongezeka barani Ulaya.

Ameitaka Urusi kutekeleza haraka mpango wa kusitisha mapigano nchini Syria, ili kuruhusu misaada ya kibinaadamu kuingia nchini humo. Steinmeier amemtaka Lavrov kushinikiza kuwepo suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Syria ulioanza mwaka 2011.

Karibu mawaziri 50 wa mambo ya nje pamoja na maafisa wa ngazi za juu wanakutana leo mjini Hamburg, katika Baraza la 23 la Mawaziri wa OSCE, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kwenye mji huo. Polisi wamesema zaidi ya maafisa wa usalama 10,000 wamepelekwa mjini humo ili kuhakikisha usalama katika mkutano huo wa ngazi ya juu.

Deutschland Vorbereitung auf das OSZE-Treffen in Hamburg
Polisi akilinda doria HamburgPicha: picture alliance /dpa/ B. Marks

Urusi na mzozo wa Crimea

Kuhusu suala la Ukraine, Steinmeier ameikosoa Urusi kwa kuhusika katika mzozo wa mashariki mwa nchi hiyo, pamoja na kuitwaa Rasi ya Crimea mwaka 2014, baada ya rais wa Ukraine aliyekuwa akiungwa mkono na Urusi, Viktor Yanukovych kuondolewa madarakani. Aidha, ameitaka Urusi ihakikishe amani inarejea barani Ulaya. Amesema wanaamini kuwa baada ya kumalizika kwa Vita Baridi, suala la vita na amani linapaswa liwe limemalizika kabisa barani Ulaya, lakini bara hilo limekuwa katika migogoro ya mara kwa mara.

''Suala la vita na amani limerejea tena barani Ulaya, baada ya Urusi kujitwalia Crimea na mpaka sasa mchakato wa amani haujazaa matunda, licha ya kuwepo juhudi kadhaa za kumaliza mzozo huo. Na kwa sababu ya hilo, ni muhimu mataifa yote ya Ulaya yakaungana pamoja kwa ajili ya mazungumzo ya ana kwa ana yatakayosaidia kumaliza mizozo barani Ulaya na nje ya bara hilo, na sio tu kutoa matamko kupitia umma,'' amesema Steinmeier.

Italien Außenminister Russland & USA Treffen in Rom Sergej Lawrovw & John Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov (Kushoto) na mwenzake wa Marekani, John Kerry (Kulia) wakiwa HamburgPicha: Reuters/G. Borgia

Muda mchache kabla ya kukutana na Steinmeier, Lavrov alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na kuzungumzia mikakati ya kumaliza mapigano kwenye mji wa Aleppo, Syria. Kerry amewaambia waandishi wa habari mjini Hamburg, kwamba wamebadilishana mawazo kuhusu Aleppo na wanadhamiria kushirikiana ili kukomesha mapigano mjini humo.

Lavrov amesema amelikubali na kuthibitisha kuliunga mkono pendekezo la Marekani la ''Disemba 2'' linalotaka waasi kujiondoa kabisa kutoka mashariki mwa Aleppo. Hata hivyo, kuna uwezekano kwamba Urusi isifikie makubaliano yoyote hadi Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump atakapoingia madarakani. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu 300,000 bado wamezingirwa ndani ya mji wa Aleppo.

 

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP
Mhariri:Hamidou  Oumilkheir