Syria kusitisha mapigano baadhi ya maeneo
29 Aprili 2016Taarifa ya jeshi la Syria imesema utaratibu mpya wa utulivu kuanzia saa saba za usiku Jumamosi utadumu kwa siku moja tu katika kitongoji cha mjii mkuu cha Ghouta na siku tatu katika viunga vya kaskazini vya jimbo la mwambao la Latakia.
Vitongoji vyote viwili vimekuwa vikishuhudia kupamba moto kwa mapambano katika siku za hivi karibuni.Hata hivyo taarifa hiyo haikuutaja mji wa Aleppo wenye mapigano makali ambao umegawika kati ya maeneo yanayoshikiliwa na serikali na yale yalioko chini ya mikono ya waasi.
Mashirika ya habari ya Urusi yamemnukuu kiongozi mmoja wa upinzani akisema kwamba suluhu hiyo mpya pia itatumika Aleppo lakini hakuna uthibitisho tafauti kuhusu hilo.
Hatua za kijeshi na matumizi ya silaha ni marufuku
Taarifa ya kijeshi ya Syria haikutowa ufafanuzi juu ya maana ya neno la "utaratibu wa utulivu " lakini shirika la habari la Interfax nchini Urusi limemkariri afisa wa kituo cha kusimamia usitishwaji mapigano cha Urusi akisema inamaanisha hatua zote za kijeshi zitasitishwa na kupigwa marufuku kwa matumizi ya silaha za aina yoyote ile.
Generali Sergei Kuralenko mwenye kusimamia kituo hicho nchini Syria pia amesema kwamba haoni hatari ya hali hiyo kugeuka kuwa mzozo kamili wa kijeshi.Shambulio la anga kwenye hospitali ilioko katika mji wa Allepo limeuwa takriban watio 30 wakiwemo watoto watatu hapo jana.
Akizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien Naibu Katibu Mkuu katika masuala ya Kibinaadamu na Mratibu wa Msada wa Dharura amesema kuna ishara nzuri sana za matumaini kwa mchakato wa kisiasa.
O'Brien) amesema "Tatizo ni kwamba watu hawawezi kuzungumza iwapo wanashambuliwa kwa mabomu, kwa bunduki za rashasha na kufa njaa.Kwa hiyo kuna haja ya kuwaelewesha watu kwamba usitishwaji wa mpigano lazima ufanye kazi vnginevyo inauyumbisha kabisa mzozo huo wa kisiasa."
Ujerumani yaonya
Serikali ya Ujerumani imesema Ijumaa shambulio katika hospitali ya Aleppo lilliouwa watu kadhaa yumkini ilikawa ni kazi ya vikosi vya serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin Steffen Seibert amesema ni ukiukaji wa wazi wa sheria ya ubinaadamu.
Serikali ya Ujerumani imeonya kwamba kupamba moto kwa mapigano huko Aleppo kunatishia kudhoofisha mazungumzo ya amani ya Geneva na kuwa hilo halina budi kuepukwa na kwamba Urusi ina wajibu wa kuzuwiya kusambaratika kwa usitishwaji wa mapigano na mchakato wa kisiasa.
Mkuu wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein naye ameyashutumu mataifa makubwa yenye kuunga mkono pande zinazohasimiana nchini Syria kwa kuwa washiriki katika umwagaji damu nchini Syria pamoja na kukiita kitendo cha kushindwa kupigania haki za wahanga wa vita hivyo kuwa cha aibu.
Kauli yake inaonekana kuikusudia Marekani yenye kuwaunga mkono makundi fulani ya waasi na Urusi mmungaji mkono mkuu wa Rais Bashar al- Assad.Serikali ya Syria inaelezea suluhu waliyoitangaza katika baadhi ya maeneo ni juhudi za kuyaokowa makubaliano ya kukomesha uhasama.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga