1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi afikishwa Mahakamani akikabiliwa na mashtaka mapya

1 Machi 2021

Kiongozi wa kiraia nchini Myanmar Aung San Suu Kyi amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka mapya yaliyofunguliwa na utawala wa kijeshi dhidi yake. Kiongozi huyo ameonekana kwenye mkanda wa vidio akiwa mwenye afya

https://p.dw.com/p/3q39i
Weltspiegel 17.02.2021 | Myanmar Militärputsch | Protest
Picha: Ye Aung Thu/AFP/Getty Images

Inaaminika kwamba mashtaka mapya yanayomkabili kiongozi huyo ni kuhisiana na uchapishaji wa taarifa ambazo zinatajwa na jeshi kwamba huenda zinaweza kusababisha hofu au wasiwasi nchini humo.

Wakili wake Khin Maung Zaw amesema Suu Kyi aliyepinduliwa madarakani na jeshi anatuhumiwa kukiuka sheria za mawasiliano pamoja na kunuia kuchochea vurugu zinazofanywa na uma wa Myanamar. Wakili huyo amesema pia kwamba hawana uhakika ni kesi ngapi nyingine zitamkabili mteja wao katika kipindi hiki kwasababu waamini hakuna kisichowezekana nchini humo.

soma zaidi: Watu 18 wauawa katika siku ya umwagaji damu Myanmar

Kiongozi huyo aliyechaguliwa na raia nchini Myanmar mwenye umri wa miaka 75 anakabiliwa na mashtaka chungu nzima ambayo Jumuiya ya kimataifa inayatilia mashaka makubwa.

Mmoja wa mawakili wake ameeleza kwamba kikao kingine cha kusikiliza kesi dhidi ya mwanasiasa huyo ni March 15. Ieleweke kwamba mwanasiasa huyu wa Myanmar alikamatwa na kuwekwa kizuizini mnamo Februari Mosi baada ya jeshi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali yake iliyowekwa madarakani na raia.

Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi bado yanaendelea Myanmar

Myanmar | Proteste nach Militärputsch
Baadhi ya raia wa Myanmar wakiandamana kupinga utawala wa kijeshi Picha: AP Photo/picture alliance

Alikamatwa mjini Naypyitaw mji ulioko nje kabisa uliojengwa na jeshi na kuufanya ndio makao makuu yake wakati wa utawala wa kidikteta uliowahi kuwepo nchini humo. Hadi leo hii San Suu Kyi hajawahi kuonekana hadharani tangu alipopinduliwa ingawa imekuwa ikiripotiwa mara zote kwamba yuko katika kifungo cha nyumbani.

Juu ya hilo bado maandamano yanaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo ambapo jana Jumapili polisi walifyetua risasi na kuwakamata watu chungunzima wakati wakiyavunja maandamano hayo. Afisa mmoja wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa amesema wanataarifa za uhakika zinazoonesha kwamba kiasi watu 18 wameuwawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika tukio hilo.

soma zaidi:Polisi Myanmar yatumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji

Idadi hiyo ya waliouwawa itakuwa ni ya juu zaidi kuwahi kutokea kwa siku moja ya waandamanaji tangu yalipofanyika mapinduzi nchini humo Februari Mosi. Inaaminika pia katika tukio la jana kiasi watu 1000 walikamatwa.

Jeshi la Myanmar limekuwa likitetea na kuhalalisha hatua yake ya kutwaa kwa nguvu madaraka kwa kutowa madai yasiyokuwa na ushahidi kuhusu kufanyika wizi na udanganyifu mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba mwaka jana.Ikumbukwe kwamba chama cha Aung Suu Kyi cha National League for Democracy NLD kilishinda kwa kishindo kwenye uchaguzi huo.

Chanzo: AFP

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW