Sudan: Makubaliano ya usitishwaji mapigano kufikia tamati
27 Aprili 2023Perthes ameliambia shirika la habari la BBC hii leo kwamba vikosi vya Sudan vimekubali mazungumzo katika mji mkuu wa Sudan Kusini wa Juba, ingawa wapinzani wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) bado hawajajibu iwapo watashiriki. Hata hivyo Perthes amesema ana uhakika RSF itashiriki kunako mazungumzo hayo.
Wakati hayo yakiarifiwa, mwandishi wa habari wa shirika la Ujerumani dpa katika mji mkuu Khartoum ameripoti asubuhi ya leo, kutokea kwa vitendo kadhaa vya majibizano ya risasi mjini humo. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, kulikuwa pia na mashambulizi kadhaa ya anga katika sehemu mbalimbali za jiji hilo ambapo majeshi ya serikali yalivishambulia vikosi vya RSF.
Soma pia: Al-Burhan aridhia mazungumzo ya IGAD
Kuhusu suala la ugavi, hali bado ni tete na inachukuliwa kuwa ya wasiwasi. Jeshi la Sudan na vikosi vya RSF, ambao hapo awali walikuwa washirika wakuu,
wamekuwa wakipigania madaraka ya nchi hiyo kwa takriban siku 10 sasa.
Mapigano makali yaripotiwa pia Darfur
Thomas Okedi, Meneja wa Baraza la Wakimbizi la Norway katika Jimbo la Darfur Kaskazini ametoa wito wa misaada zaidi.
"Sasa ni siku kumi na moja. Siku kumi na moja za mateso, siku kumi na moja za watu kufa, siku kumi na moja za familia kukosa chakula, siku kumi na moja za watoto kuishi katika hali isiyo na matumaini, siku kumi na moja za kukata tamaa. Ni muhimu ulimwengu usimame na watu wa Sudan, kutoa rasilimali zinazohitajika kwa mashirika ya kibinadamu ili kuongeza misaada ya kibinadamu kwa watu wanaohitaji."
Muda wa masaa 72 ya usitishaji mapigano unamalizika jioni ya leo Alhamisi. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mpango wa mazungumzo uliyosimamiwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Afrika Mashariki (IGAD).
Katibu mtendaji wa shirika hilo la IGAD Workneh Gebeyehu amesema leo kwamba ana uhakika juhudi mbalimbali za jumuiya ya kimataifa zitasaidia kukomesha mapigano na kuupatia suluhu mzozo huo.
Soma pia: Sudan: Mkuu wa majeshi aashiria kulikubali pendekezo la IGAD la kuongeza muda wa kusitisha mapigano
Muda mfupi baada ya kuzuka kwa ghasia mjini Khartoum, marais kutoka Sudan Kusini, Kenya na Djibouti walipendekeza kuwa wapatanishi lakini hatua hiyo ilisitishwa kutokana na ukosefu wa usalama katika mji mkuu wa Sudan.
Hadi sasa juhudi kadhaa za usuluhishi zimefeli tangu kuzuka kwa mapigano Aprili 15 kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na naibu wake aliyegeuka kuwa mpinzani, Mohamed Hamdan Dagalo.